Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Timu ya Dodoma FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania leo imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ngumu ya ligi kuu Lipuli FC ya Iringa katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Ikiwa ni mchezo wa pili wa majaribio kwa Dodoma FC baada ya mchezo wa kwanza kutoka suluhu ya kutokufungana na Mbeya city, ili shuhudiwa hadi kipindi cha kwanza kinamalizika bila kufungana huku Dodoma FC wakiwa pungufu baada ya mchezaji wao kiungo Rajabu Saif, kutolewa kwa kadi nyekundu.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikifanya mabadiliko ya hapa na pale kuhakikisha wanaibuka na ushindi, lakini bahati ilikuwa kwa Dodoma FC, licha ya kuwa pungufu walipata bao lililofungwa na mshambuliaji wao hatari Anuary Jabir.
Lipuli walifanya jitihada za kurejesha bao hilo lakini uimara wa timu ya Dodoma FC inayofundishwa na Mbwana Makata, walikuwa imara kulinda lango lao, hadi mwisho wa mchezo.
Mara baada ya mchezo huo kocha wa Lipuli Haerman Haruna, amesema mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho kwao katika maandalizi ya mitanange wa ligi kuu, inayoanza mwishoni wa wiki hii, ambapo wataanza dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, amesema ameridhishwa na kiwango cha wachezaji wake kwani walikuwa wakicheza kuhofia majeruhi.
“Timu yangu amecheza vizuri licha ya makosa ya hapa na pale ambayo ni ya kawaida nadhani hawajacheza kwa nguvu wanahofia majeruhi kama unavyojua ligi inaanza hizi karibuni” amesema Haerman.
Nae Kocha wa Dodoma FC Mbwana Makata amesema michezo hiyo miwili imekuwa kipimo sahihi kwa timu yake kwani timu alizocheza nazo ni kubwa, na timu yake amecheza vizuri na amesema watacheza na Mtibwa ya Morogoro katika mchezo wa mwisho baada ya hapo atacheza na timu ya ligi daraja la kwanza na hicho ndio kitakuwa kipimo sahihi kwake.
