Na John Walter-Babati
Mbunge wa Babati Mjini mkoani Manyara, Paulina Gekul ametoa mifuko 100 ya saruji ili kusaidia katika ujenzi na ukarabati wa shule za Msingi ikiwa ni harakati za kuhakikisha elimu inatolewa kwa ubora katika jimbo lake.
Amesema aliomba msaada wa kupata saruji kutoka shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kurekebisha miundo mbinu ya shule mbalimbali za msingi ambazo zimekuwa kongwe.
Mh. Gekul amekabidhi mifuko hiyo leo kwa viongozi wa mitaa ya Sawe,Komoto na Himiti huku akisisitiza zikatumike vizuri kwa kazi iliyokusudiwa.
Shule zilizonufaika na msaada huo wa saruji ni shule ya Msingi Sawe ambayo ni mpya iliyopata mifuko 33 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa madarasa,Himiti 52 na Komoto imekabidhiwa mifuko 15 kwa ajili ya kufanya ukarabati .
Viongozi waliokabidhiwa Mifuko hiyo ya Saruji wamempongeza Mhe Gekul kwa kazi kubwa anayofanya katika kuwatumikia Wananchi wa jimbo lake kwa kuboresha miundo mbinu ya shule,bara bara na nyingine ambazo ni muhimu kwa jamii.
Naye meneja wa shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Manyara na Arusha Ladislaus Bamanyisa, amesema shirika lao lina sera ya huduma kwa jamii ambapo wanashiriki katika shughuli za maendeleo katika taasisi za kijamii kwa kutoa misaada mbalimbali na wamefanya hivyo Babati ikiwa ni ombi la Mbunge huyo.