Watu 11, mbaroni kwa tuhuma za mauaji

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu 11, kwa tuhuma za kujihusisha na mauaji ya mtu mmoja aitwaye Samweli John (26) Msukuma Mkazi wa Kijiji cha Migombani Luhama wilayani Sengerema, baada ya kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na mawe na kundi la wannachi waliojichukulia sheria mkononi wakati alipokuwa amehifadhiwa katika ofisi ya mwenyekiti wa serikali ya kijiji  cha Bulyahiru baada ya kukamatwa kwa tuhuma za wizi wa mkungu wa ndizi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ACP Muliro Muliro, amesema kuwa tukio hilo limetokea baada mwenyekiti wa kijiji hicho kuanza kuwazuia watu hao, ambao walianza pia kumshambulia alipowasiliana na polisi ili wafike kumchukua, pia polisi walifika walianza kushambuliwa na hivyo kulazimika kumuokoa mwenyekiti baada ya mtuhumiwa kukutwa ameuawa.

Muliro ameeleza kuwa Askari NO D 9777 SGT Juma alijeruhiwa kwa jiwe kichwani na Mwenyekiti Benjamini Kahitira, aliumia kwenye paji la uso na watu wawili ambao ni Dorica Majingo alijeruhiwa kwa risasi kwenye paja la mguu wa kulia na Musa Mange alijeruhiwa kwenye goti la kushoto kwa risasi baada ya kuwashambulia askari polisi kwa mawe ambapo majeruhi walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa matibabu.

Aidha Kamanda Muliro ametoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi waache mara moja kwani ni kosa la jinai ambapo kwa yeyote atakayebainika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mpya zaidi Nzee zaidi