Serikali yazindua mpango kazi wa kuendeleza Miji Tanzania



Na,Enock Magali,Dodoma.

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Seleman Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa kote nchini  kuusimamia Mpango kazi wa kuendeleza Miji Tanzania,aliouzindua hii leo Jijini Dodoma.

Akizindua Mpango kazi huo,Waziri Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuusimamia mpango huo ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo husika.

"Niwaombe wadau tujipange kwenda kutekeleza mpango huu na niwaombe,Wakuu wa Mikoa kuanisha eneo kwa eneo ikiwa ni pamoja na kuusimamia," alisema.

Jafo amesema kwa sasa ongezeko la watu ni kubwa hususa ni katika Mikoa ya Dodoma na Dar es salaam hivyo akadai kwamba mpango kazi huo umekuja wakati muafaka.

"Bila kuwa na mpango kazi inawezekana tukaishi maisha sio mazuri,mabadiliko haya ambayo yanafanywa sasa hivi ni muhimu sana katika upangaji wa miji," alisema.


Waziri Jafo amesema  Mji wa Dar es salaam upo hovyo na haujapangika vizuri hivyo akataka isitokee tena kwenye miji mingine.

"Mji wa Dar upo hovyo,hata moto ukitokea hauwezi kuokoa tujiulize ni majanga mangapi yametokea tumeshindwa kuokoa sababu ya Miji kupangwa vipaya ?

" Jiji la Dar tumechelewa yaani unatamani uchukue Greda uvunje nyumba kwani zimekaa vibaya.Niwapongeze Dodoma angalau Jiji limekaa vizuri,"alisema Jafo.

Aidha,alisema lazima Miji ipangwe vizuri kwani kwa sasa ile ambayo imepangwa vizuri imeweza kusababisha kuongezeka kwa mapato kutokana na Serikali kuweza kukusanya kodi.

"Sehemu zingine gari la zimamoto haliwezi kupitia,sehemu zingine kupitisha jeneza shida,msiba unakuwa nyumba ya tatu sababu kwenye msiba hakufikiki.Kuna vijana wana magari mazuri lakini yanakaa kwa jirani wanapokaa hakufikiki," alisema.

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Angelina Mabula alisema mpango huo ni muhimu na utasaidia katika ujenzi wa Miji iliyopangika pamoja na kuongeza thamani ya ardhi.

Mabula alisema Serikali  imetayarisha Mipango kabambe 30 kwa mwaka 2018-2019 ambapo 20 imekamilika huku 10 ikiwa katika mipango mbalimbali.

Naye,Naibu Katibu Mkuu,Wizara ya Fedha na Mipango,Adolf Ndunguru alisema kwa sasa Miji inakuwa hivyo mpango huo umekuja wakati muafaka.