https://monetag.com/?ref_id=TTIb Wakurugenzi walioshindwa kukusanya mapato kupewa vinyago vya uzembe | Muungwana BLOG

Wakurugenzi walioshindwa kukusanya mapato kupewa vinyago vya uzembe


Na Ezekiel Mtonyole-Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ametoa wiki mbili kwa halmashauri  zote zilizokusanya mapato chini ya asilimia 50 ya malengo yao kuandika barua ya kujieleza kwa Katibu Mkuu TAMISEMI  ya kwanini wasichukuliwe hatua kwa kutofikia malengo.

Pia amesema Wakurugenzi walioshindwa kukusanya mapato watapewa vinyago vya uzembe na kutofikia lengo kisha kutakiwa kuviweka mbele ya ofisi zao na za wakuu wa mikoa hiyo.

Amebainisha kuwa agizo hilo pia limewahusu wakurugenzi kutoka halmashauri zaidi ya 40 walioshindwa kutoa fedha za mikopo kwa kwa makundi ya vijana, walemavu na wanawake chini ya asilimia 50 zilizotakiwa kutengwa.

Hayo ameyabainisha Jijini Dodoma wakati akizungumza na Wanahabari, Waziri Jafo amezitaja halmashauri ambazo wakurugenzi wake watapewa vinyago kwa kushindwa kukusanya mapato.

“Vinyago nitakavyovitoa  vitakuwa na sura mbaya sana na Wakurugenzi wa halmashauri hizo wanatakiwa kuviweka kwenye ofisi zao na ofisi za wakuu wa mikoa husika,” amesema.

“Halmashauri ambazo zitahusika zilizoshika mkia kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa (pato ghafi) ni  Halmashauri za Wilaya za Kakonko (Sh. milioni 408.2), Buhigwe (Sh. milioni 403.8), Kigoma (Sh. milioni 397.1), Gairo (Sh.milioni 396.2) na  Halmashauri ya Mji wa Nanyamba (Sh. Milioni 257.6)” amesema.

Amezitaja halmashauri za mwisho kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa ukilinganisha na makisio ya halmashauri ya mwaka ni Halmashauri za Wilaya za Newala (27%), Masasi (26%), Msalala (19%), Tandahimba (19%) na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba (11%).

Pia amebainisha kuwa kuna uwepo wa Halmashauri zaidi ya 40 ambazo zimeshindwa kuchangia katika Vikundi vya Wanawake, Vijana, na Watu wenye Ulemavu.

“Nataka na hawa nao wajieleze sababu za kushindwa kusimamia Kanuni za Usimamizi wa Fedha za michango ya Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu,”  amesema.

Waziri Jafo amezitaja halmashauri tano zilizoongoza kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa (pato ghafi), Jiji la Dodoma limeongoza kwa kukusanya sh. bilioni 71.7, Halmashauri za Manispaa za Ilala sh. bilioni 58.2, Kinondoni (Sh.Bilioni 34.0), Temeke (Sh. Bilioni 33.3) na Ubungo (Sh. Bilioni 18.6).

“Mikoa iliyoongoza ni Dar es Salaam (Sh. Bilioni 163.6), Dodoma (Sh. Bilioni 82.7), Mwanza (Sh. Bilioni 32.7), Arusha (Sh. Bilioni 31.9) na Mbeya (Sh. Bilioni 31.4)” amesema Jafo.

Ameitaja mikoa mitano ya mwisho kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa (pato ghafi) ni Njombe (Sh. Bilioni 11.5), Simiyu (Sh. Bilioni 8.8), Rukwa (Sh. Bilioni 8.2), Kigoma (Sh. Bilioni 7.8) na Katavi (Sh. Bilioni 7.4).