Wananchi wagomea ujenzi wa shule kwa madai ya watu kupotea


Na Amiri kilagalila-Njombe

Wakazi wa kijiji cha Itulahumba wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe wamepinga vikali pendekezo la wataalamu wa Halmashauri na uongozi wa kata ya Itulahumba la ujenzi wa shule ya Sekondari ya kata katika kitongoji cha Lwipula kijiji cha Isakalenga kwa madai ya kwamba sio salama kwa watoto kwani watu wamekuwa wakipotea mara kwa mara katika eneo hilo.

Mbali na changamoto ya usalama, wamedaiwa kuwa kijiji cha Isakalenga kinachangamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, maji, afya na umeme ikilinganishwa na vijiji vingine vitatu kikiwemo cha Itulahumba, Ihanzutwa na Isindagosi ambavyo vinaunda kata hiyo jambo ambalo linawafanya kuiomba serikali kubadili eneo la ujenzi kutoka kijiji cha Isakalenga hadi Itulahumba ambayo inafikika na vijiji vyote.

Diwani wa kata hiyo Thobias Mkane amejibu madai hayo kwa kusema hakuna jambo linalofanyika ambalo halipo kwenye vikao halali.

"Wasiweke ajenda nyingine ila kama wanagomea maendeleo kwamba hatutaki kujenga sekondari hatutaki kuungana na hivi vijiji vitatu ambavyo vinaendelea kutoa michango na sasa hivi wametoa milioni 13 tunazo waseme lakini sio kukwamisha jambo kwa kuweka  kitu ambacho kinahatarisha amani”alisema diwani

Kufuatia mgogoro huo wananchi hao wamekubaliana katika mkutano huo kutoshiriki ujenzi huo ambao wamedai utawapa wakati mgumu watoto wao na kumuomba mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka kufika kijijini kwao kumaliza mgogoro huo.