Watanzania watakiwa kuamka katika zao la Parachichi


Na Amiri kilagalila-Njombe

Kilimo cha parachichi kimeendelea kukua Tanzania hususani katika mikoa ya nyanda za juu kusini ukiwemo Njombe, Mbeya na Iringa na kuchangia pato kubwa la taifa licha ya changamoto ya soko la moja kwa moja likiendelea kuwa tatizo.

Kutokana na changamoto hiyo wataalamu wa kilimo kutoka nchini Kenya wamesema njia pekee ya kukabiliana na tatizo la nchi yao kugonga nembo ya Kenya kwa mazao yanayozalishwa Tanzania ni wakulima kuunda vyama vikubwa na vyenye nguvu vitakavyokuwa na uwezo wa kwenda nchi za ulaya ambako soko liliko kutafuta mitandao ya masoko itakayowasaidia kulifikia soko moja kwa moja bila kupitia Kenya.

Ushauri huo umetolewa mkoani Njombe na mtaalamu wa kilimo kutoka nchini Kenya Joseph Musuya alipokutana na wakulima wa parachichi kujadili mstakabali wa soko la malighafi hiyo ambayo uhitaji wake soko umeendelea kukua kila uchwao ambapo amesema Wakenya wanapata faida kubwa kupitia mazao ya Tanzania kwani wamekuwa wakinunua kwa bei nafuu na kuyauza kama zao la Kenya bei ya juu hatua ambayo inakuza pato la wanunuzi na taifa kwa ujumla.

Awali akitoa ushauri kwa wakulima Frank Msigwa ambaye ni mwenyekiti wa mtandao wa wakulima wa parachichi mkoani Njombe NISHIDA amesema wakulima wanapaswa kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake wafanye kilimo biashara ili kuwa na uhakika wa soko la kimataifa badala ya kutegemea wanunuzi wa Kenya.