Na Thabit Madai,Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Siri kubwa ya mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya Tasaf Zanzibar ni uratibu na usimamizi mzuri wa fedha zinatolewa katika kutekeleza miradi hiyo.
Amesema Ofisi yake imekuwa ikiratibu na kusimamia vizuri matumizi ya fedha za miradi ya Tasaf na kupelekea kufanikisha vyema Miradi hiyo ya Maendeleo ya Jamii.
Kauli hiyo Balozi Seif alito wakati wa Mazungumzo yake na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria waliowasili Zanzibar kwa ziara ya Siku mbili kuja kujifunza kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mpango wa kuhudumia Kaya Maskini Nchini Tanzania.
Balozi Seif alibainisha kwamba ofisi yake ndio inayoratibu shughuli zote za Tasaf kwa upande wa Zanzibar imelazimika kuchukuwa hatua hiyo ili kulinda Heshima itakayotoa ushawishi kwa Wafadhili wa Mpango huo kuendelea kuunga mkono katika utoaji wa Mikopo zaidi.
Alieleza kwa vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} unatoa huduma katika pande zote mbili za Tanzania, Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinalazimika kufuatilia mwenendo mzima wa fedha zinavyotumika katika Miradi ya Tasaf ili kufikia lengo.
“Serikali ililazimika kufanya uchambuzi yakinifu na kujiridhisha katika mwenendo wa wa matumizi ya Miradi ya Tasaf ili kuepuka upotevu ambao ungegharimu machungu kwa wasimamizi wa Miradi hiyo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alisema ipo Miradi mingi ya Kijamii katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba Mjini na Vijijini iliyoleta ukombozi kwa Wananchi walio wengi baada ya kupata msukumo uliotokana na uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania katika Awamu tofauti uliojikita kuhudumia moja kwa moja miradi hiyo.
Balozi Seif alisema ipo haja kwa Wafadhili wa Miradi ya Kijamii akatolea Mfano Benki ya Dunia pamoja na Taasisi nyengine za Kimataifa za misaada ya Maendeleo kuendelea kuongeza ufadhili wao kwa vile lengo la uanzishwaji wa Miradi ya Kijamii limefanikiwa vyema.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hatua hiyo ya Wafadhili ni muhimu kwa vile inaweza kusaidia kuondoa mkwamo kwa baadhi ya Changamoto zinazotokana na Miradi inayoanzishwa hasa katika Sekta za uzalishaji kupitia Vikundi vya ujasiri amali.
Balozi Seif aliishauri Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa Majimbo ya Nigeria kwamba katika kuimarisha Miradi na huduma za Kijamii ipo haja ya Mataifa ya Afrika kuzidi kushirikiana katika kubuni mbinu na njia za pamoja katika kuendeleza Miradi hiyo itakayoleta ustawi na Maisha bora kwa Waafrika walio wengi.
Alisema mfano ulioonyeshwa na Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria wa kufika Tanzania kujifunza mwenendo wa uendeshaji wa Miradi ya Kijamii ni mwanzo wa kuigwa kwa Mataifa mengine yanayotekeleza Miradi kama hiyo Barani Afrika.
Mapema Mratibu wa Washirika wa Sekta za Kijamii kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wa Nchini Nigeria Bwana Gyangyang Limave ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa umakini wake iliyonao wa kuhakikisha Bara la Afrika linaendelea kuimarika Kiuchumi na Ustawi.
Bwana Byangyang alisema msimamo wa Tanzania katika kustawisha maisha ya Wananchi wake ni mfano wa kuigwa na Mataifa mengine Duniani yaliyoanza mpango wa kuimarisha Taasisi za Kijamii.
Alisema Serikali ya Nigeria katika muelekeo wake wa kustawisha Maisha ya Wananchi wake tayari imeshaanzisha Taasisi inayoratibu na kusimamia kasuala ya Kijamii mnamo Mwaka 2016.
Bwana Gyangyang Limave alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.3 zimetolewa na Serikali Kuu katika kuimarishaji wa Kaya Maskini Nchini humo.


