Afisa Habari wa timu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amewapongeza waamuzi waliochezesha mchezo wa ligi kuu kati ya timu hiyo na Tanzania Prisons, uliopigwa jana Septemba 15, 2019 kwenye Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya na Ruvu kuchezea kichapo cha mabao 2-1.
Masau amesema waamuzi wa mchezo huo Rafael Ikambi wa Morogoro na wasaidizi wake, Martin Mwaliaje na Nestory Livangala, wote kutoka Tabora walifanya kazi nzuri wakichezesha kwa kuzingatia sheria, uwezo mkubwa, walijua kuzitafsiri sheria 17 za soka na walitenda haki kwa kila timu.
“Ningekuwa mimi ndiye natoa Beji, jana baada ya mchezo wote hao ningewavisha BEJI ya FIFA. Nawapa sana KONGOLE, waendelee kuchezesha kwa haki michezo yao yote”, amesema Masau.
Akizungumzia matokeo waliyoyapata kwenye mchezo huo, Masau amesema licha ya kuonekana kuwa ya ajabu kwa wengi, wao kama Ruvu Shooting wanaamini yatawafikisha kwenye mafanikio ya kisoka waliyokusudia msimu huu.
Amesema licha ya kufungwa, timu yao ilionesha kiwango kikubwa kuliko wapinzani wao hivyo hawajajuta wala kuumizwa na matokeo wakiamini kuwa ili wafikie mafanikio ni lazima wapiti changamoto za aina hiyo.
“Kumbuka, Yona hakufika Ninawi kwa raha, alipata shida kubwa, siku tatu yumo ndani la tumbo la samaki anasafiri kuelekea Ninawi. Mwisho wa siku tunaona Yona anafanikiwa kuwakomboa watu wa Ninawi”, amesisitiza.
Agosti 28 mwaka huu baada ya kuifunga Yanga bao 1-0 kwenye Uwanja wa uhuru Dar es Salaam, Masau alisema kwa ubora walionao, Ruvu Shooting ndiyo watakaokuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
