Mikoa 13 inakabiliwa na panya wanaoharibu mazao


Bunge limeelezwa kuwa mikoa 13 nchini imekuwa ikikabiliwa na milipuko ya panya wanaoshambulia mazao.

Kufuatia hali hiyo, Halmashauri ambazo hupata milipuko hiyo mara kwa mara zimetakiwa kutenga bajeti kwa ajili ya kushirikiana na Wizara ya Kilimo kufanya udhibiti endelevu wa mnyama huyo.

Kauli hiyo ilitolewa  Bungeni na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akijibu swali la Mbunge wa Malinyi(CCM), Dk. Haji Mponda ambaye amehoji serikali ina mkakati gani wa kusambaza sumu maalum ya kuuwa panya hao.

"Kwakuwa upatikanaji wa sumu ya panya una changamoto nyingi, Serikali ina mkakati gani mbadala katika kukabiliana na panya waharibifu wa mazao shambani,"amehoji.

Amesema wilaya hiyo tangu mwaka 2014 inakabiliwa na mlipuko wa panya wanaoshambulia mbegu za mazao ya mpunga na mahindi katika kipindi cha upandaji.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Bashe alisema visumbufu vya mazao wakiwemo panya husababisha upotevu wa mazao nchini.

Ametaja mikoa ambayo inakabiliwa na panya kuwa ni Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya, Songwe, Iringa, Pwani, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mwanza na Morogoro ikiwemo wilaya ya Malinyi.

"Wakulima wana wajibu wa kupambana na panya katika mashamba yao wakati wote wa kutumia mbinu husishi wakiwa wachache,"amesema.

Aidha amesema inapotokea panya kuongezeka hadi kufikia zaidi ya 700 kwa ekari, Serikali huratibu ugawaji wa sumu kali kwa wakulima ambayo ina uwezo wa kudhibiti panya kuanzia dakika 45 hivyo kuzuia ukuaji wa mbegu.