Wanaume wametakiwa kuacha mfumo dume kwa wake zao


Wanaume wametakiwa kuacha mfumo dume kwa wake zao wanaotaka kugombea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, badala yake wawaunge mkono ili wagombee.

Kauli hiyo ilitolewa na madiwani wa viti maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Mtera na Chilonwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya madiwani wenzake wa viti maalumu, Hilda Kadunda Diwani wa Iloje amesema kumekuwepo na tabia kwa wanaume kuendekeza mfumo dume ambao umekuwa ukiwanyima haki ya kimsingi ya kugombea nafasi za uongozi wanawake zao.

Amesema wanawake wana uwezo wa kuongoza lakini wananyimwa haki zao za kimsingi za kuwa viongozi kwa dhana potofu kuwa atakuwa akifanya mambo mabaya tofauti na malengo aliyogombea nafasi hiyo.

"Imani kama hiyo kimsingi ni mfumo dume imepitwa na wakati ukizingatia kuwa wanawake wanaweza kuongoza, wengi wetu ni wabunifu, hivyo ni muhimu wakapewa nafasi za kuongoza kwa kuwa watakuwa wanafuata kanuni na misingi bora ya chama husika anachongombea,"amesema.

Diwani huyo pia aliwataka wanawake kwa upande wao wajishughulishe kwenye ujasiriamali na shughuli nyingine za kiuchumi zitakazowaletea mapato ya kiuchumi ili waweze kuaminiwa na wanaume ambao wanaofikiri kuwa akin mama ni dhaifu.

Diwani wa Dabalo viti maalumu Fatuma Semninga aliwataka wanawake wenye sifa ya uongozi kutowaachia akina baba kugombea peke yao na wao kuishia kuwafanyia kampeni, badala yake wajitokeze kwa wingi ili kuzishika nafasi hizo.

Alisema badala ya kuishia kuwapigia kampeni akina baba kwenye uchaguzi huo wa serikali za mitaa, ni wakati wao pia kujitokeza kwa wingi kugombea na kupiga kura.

"Nawaomba wanawake wezangu wa jimbo la Chilonwa na Mtera mjitokeze kwa wingi ikiwa na pamoja na kupiga kura, badala ya kutumiwa kufanya kampeni kwa wagombea wengine ni wakati sasa wakatumia fursa hiyo wakachukua hatua ya kugombea," alisema Diwani huyo aliwataka wanawake kuunda vikundi vitakavyowawezesha kukokopeshwa ili kupata mikopo itakayowainua kiuchumi.