Wagombea wawili wajitoa kwenye kinyang'anyiro cha urais Tunisia

Wagombea wawili wa uchaguzi wa rais nchini Tunisia wameamua kujitoa na badala yake kumuunga mkono waziri wa ulinzi Abdelkarim Zbidi, mgombea wa kujitegemea anaeungwa mkono na chama cha Nidaa Tounes, kiliochoshinda uchaguzi wa mwaka 2014.

Waziri wa zamani Mohsen Marzouk na mfanya biashara Slim Riahi wametangaza kujitoa mashindanoni kupitia mtandao wa Facebook muda mfupi kabla ya kampeni za uchaguzi kumalizika saa sita za usiku jana.

Wote wawili ni miongoni mwa wagombea wenye mafungamano na chama cha Nidaa Tounes. Mohsen Marzouk amechapisha picha mtandaoni akiwa pamoja na Zbidi akisisitiza ameamua kujitoa ili "kuiepushia nchi yao balaa la kuongozwa wafuasi wa itikadi kali." Miongoni mwa vigogo katika uchaguzi huo wa rais ni pamoja na Nabil Karoui aliyekamatwa kwa tuhuma za utakatishaji fedha na kiongozi wa chama cha itikadi kali Ennahda, Abdelffatah Mourou. Wapiga kura milioni saba wa Tunisia wanatakiwa kupiga kura kesho Jumapili kumchagua rais wao.