Waziri Mkuu atoa agizo zito Wizara ya Maji


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji ifuatilie utendaji wa Mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini na ihakikishe kwamba bili wanazotozwa wananchi zinakuwa na uhalisia na si kuwaumiza.

Ametoa agizo hilo baada ya kuibuka wimbi la malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu upandaji wa bili za maji ambao hauna uhalisia kwa sababu Serikali ndiyo inayotoa fedha za miradi hiyo nchini.”Serikali haitakubali wala haitoruhusu mwananchi anatozwa gharama kubwa za maji.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbungewa Viti Maalumu, Mariam Kisangi, aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu suala hilo.

“Yako maeneo ambayo mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maji kumejitokeza wimbi la mabadiliko ya kuhusu kupanda kwa bei za bili, mfano wilayani Maswa mkoani Simiyu bei imeongezeka kutoka sh. 5,000 hadi 28,000 kwa mwezi.”

“Bei hizo hazina uhalisia na hakuna sababu ya mamlaka kuzoza bei kubwa kiasi hicho na kuwafanya wananchi washindwe kumudu kulipia bili zao, wakati Serikali ndio imetoa fedha za kugharamamia uanzwishwaji wa miradi hiyo na haijadai kurudishiwa fedha hizo.”

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ifuatilie bei za bili wanazotozwa wananchi ili kujiridhishwa kwamba zinazingatia uwezo wa wananchi wengi kuzilipa hasa wale wa vijijini.