Na Mwaandishi Wetu.
Wazee wa mila wa koo 12 za kabila la Wakurya wilayani Tarime, mkoani Mara, wamekemea vikali kitendo cha John Heche kukiuka mila na desturi za Kikurya, hususan mila ya kuwaheshimu wazee na viongozi wanaolingana na wazazi wake. Wamesema tabia hiyo ya kuwadharau na kuwadhalilisha viongozi wakuu inaweza kuleta madhara katika familia yake na jamii kwa ujumla.
Akizungumza mbele ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Maganya Abdallah Rajabu, aliyekuwa Tarime kwa ziara ya kichama, mmoja wa wazee hao, Julius Nyang’era, alisema wazee wameendelea kusimamia amani katika jamii licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza.
“Sisi wazee wa kabila la Wakurya tuna mila na desturi nzuri ambazo tunapaswa kuzienzi na kuzilinda. Tunamuomba kijana wetu John Heche aache mara moja tabia ya kukiuka mila ya kuwaheshimu wazee wanaolingana na baba yake mzazi. Mfano ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Steven Wasira, ambaye amekuwa akimtukana na kumdhalilisha. Aache tabia hiyo, vinginevyo anajiletea laana katika nyumba yake na familia yake,” alisema Julius.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Tarime, Sameli Mangaraye, alisema wazee ni tunu ya Taifa na wanapaswa kuheshimiwa kutokana na uzoefu na mchango wao katika kujenga familia, jamii na Taifa, pamoja na kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Maganya Abdallah Rajabu, alisema John Heche amekiuka mila na desturi za Wakurya kwa kuwadharau na kuwatukana viongozi pamoja na wazee wanaolingana na wazazi wake.
Maganya alisisitiza kuwa kuna haja kwa kiongozi huyo kuomba msamaha hadharani, akionya kuwa jamii haitakuwa tayari kuendelea kukaa kimya wakati viongozi na wazee wanadhalilishwa.
“Jamii ya Wakurya inapaswa kudumisha mila na desturi zetu nzuri, lakini pia tunapaswa kupinga mila zilizopitwa na wakati. Hata hivyo, hatuko tayari kuona viongozi wetu wanatukanwa na kudhalilishwa,” alisema Maganya.
Aliongeza kuwa hata katika mazingira ya kutokubaliana kisiasa, viongozi wanapaswa kuheshimiana na kutumia lugha inayozingatia heshima na hadhi ya viongozi wa Taifa.
“Hatuko tayari kuona viongozi wetu wanatukanwa na kudhalilishwa, akiwemo Rais wetu, Samia Suluhu Hassan. Tunamuomba Heche kwamba hata kama hatambui Serikali ya Samia, anapaswa kumheshimu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumtaja kwa heshima anayostahili, si vinginevyo,” alisisitiza Maganya.
