Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko la bunifu zinazolenga kutatua changamoto za wananchi, huku Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) ikieleza dhamira ya kuendelea kuwawezesha wabunifu na watafiti nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa COSTECH, Amos Nungu, amesema hayo wakati akizungumza kuhusu bunifu zinazooneshwa katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.
Nungu amesema maonesho hayo yamekuwa fursa ya wananchi kuona kwa vitendo namna watafiti na wabunifu wazawa wanavyotumia teknolojia kutengeneza suluhisho katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Amesema miongoni mwa bunifu zilizovutia ni kifaa kinachowekwa kwenye sikio la ng’ombe kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa afya ya mnyama.
“Teknolojia hii inamwezesha mfugaji kufuatilia afya ya mnyama na kufanya maamuzi kwa wakati, jambo ambalo linaweza kusaidia kuongeza tija katika ufugaji,” amesema Nungu.
Katika eneo la kilimo na usindikaji, Nungu ametaja ubunifu unaofanywa na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela African Institution of Science and Technology, ambapo mtafiti aliyewahi kupata ufadhili wa COSTECH ametumia maganda ya korosho kutengeneza bidhaa ya kulainisha ngozi.
Amesema ubunifu huo umeendelea kutoka hatua ya utafiti hadi kufikia kuwa na kiwanda ndani ya chuo, akieleza kuwa mafanikio hayo yanaonesha matokeo ya uwekezaji katika tafiti na ubunifu.
AI yaingia kwenye sekta ya ufugaji samaki
Nungu amesema COSTECH pia imekuwa ikitoa ufadhili kwa bunifu zinazotumia akili unde (Artificial Intelligence), hatua iliyowezesha kutengenezwa kwa teknolojia mbalimbali za kukabiliana na changamoto za jamii.
Ametaja programu tumizi inayosaidia kutambua magonjwa ya samaki kama moja ya matokeo ya uwekezaji huo, hususan kwa wafugaji wanaotumia mfumo wa vizimba.
Kwa mujibu wa Nungu, matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kusaidia wafugaji kubaini matatizo ya afya ya samaki mapema na kuchukua hatua stahiki.
Wananchi watakiwa kuunga mkono wazawa
Kutokana na bunifu hizo, Nungu amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo ili kujifunza, kuona bidhaa zinazozalishwa na wabunifu wazawa na, pale inapowezekana, kuzinunua.
Amesema kununua na kutumia bidhaa zinazotokana na bunifu za ndani ni njia mojawapo ya kuwaunga mkono wabunifu na kuwapa nafasi ya kukuza biashara zao.
COSTECH yaweka mkazo kwa uwekezaji
Akizungumzia miaka 40 ya COSTECH, Nungu amesema taasisi hiyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watafiti na wabunifu kupitia ufadhili pamoja na mijadala na majadiliano yatakayosaidia kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kupanga hatua zinazofuata.
Amesema COSTECH pia itaongeza juhudi za kuwatangaza wabunifu na bunifu zao ili kuwafikia wawekezaji, hatua inayolenga kuzifanya bunifu hizo zitoke katika hatua ya maonesho na kufikia uzalishaji na matumizi mapana zaidi.


