Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepanga kutoa hukumu Ijumaa October 11,2019 dhidi ya Kigogo wa TPRI, Aresteric Silayo anayedaiwa kumbaka mwanae wa kike mwenye umri wa miaka 11.
Hayo yamebainishwa Mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Aziza Temu aliyepewa Mamlaka na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kusikiliza rufani za pande zote mbili.
Awali Wakili wa Serikali Azael Mwiteni aliiomba Mahakama hiyo kutengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ya kumwachia huru mtuhumiwa huyo kwakuwa ushahidi wa Mtoto unaonesha alibakwa na Baba yake kwani Mtoto alimweleza Mwalimu shuleni, Mahakamani na pia cheti cha Daktari aliyemchunguza amethibitisha Mtoto kubakwa.
"Katika ushahidi huo Mwalimu alieleza alimkuta Mtoto huyo amelala darasani wakati wa vipindi na alipomwita ofisini na kumuuliza sababu za kulala na kutoweza kutembea vizuri alimjibu Baba yake humfanyia tabia mbaya asubuhi kabla ya kwenda shuleni mara kwa Mara"
