https://monetag.com/?ref_id=TTIb Naibu Waziri ataka mawasiliano yatumike kupunguza maambukizi ya UKIMWI | Muungwana BLOG

Naibu Waziri ataka mawasiliano yatumike kupunguza maambukizi ya UKIMWI


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amezitaka kampuni za simu za mkononi kuweka ujumbe au tangazo kwenye simu za wateja kwa lengo la kuendesha kampeni ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa wananchi.

Nditiye ameyasema hayo akiwa kwenye kikao na viongozi wa kampuni hizo mkoani Mwanza na kuwataka watengeneze na kuweka ujumbe au tangazo hilo kuanzia tarehe 15 Oktoba mwaka huu hadi Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Ugonjwa wa UKIMWI yanayofanyika tarehe mosi Novemba kila mwaka ambao utawakumbusha wananchi kuwa UKIMWI bado upo, ni janga la kitaifa na hauna dawa

“Ninyi ni mawasiliano na mawasiliano yananihusu, sisi tunapatikana kila dakika kuliko televisheni, redio au magazeti, kila mwananchi anapatikana kwa kuwa ana simu ya mkononi na ninyi mtusaidie kutangaza masuala ya kimkakati ya kitaifa mfano janga la UKIMWI bado lipo, mtusaidie kuweka ujumbe kuhusu ugonjwa huu ili tusaidie wananchi,” amesema Nditiye

“Ikilazimika mtume hata ujumbe kuhusu ugonjwa huu ili ujumbe huo uanze kusikika kwa kuwa watanzania ni wateja wenu wakubwa tuwahudumie na wenye simu wengi ni watu wenye uwezo na kwa bahati mbaya ndio wanaopatwa na majanga ya magonjwa haya na hao ndio wateja hivyo tuwasaidie,” amesisitiza Nditiye

Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Vodacom, Gwamaka Mwakilemba amemweleza Nditiye kuwa wako tayari kuandaa ujumbe au tangazo hilo kwa kuwa janga la UKIMWI linagusa jamii ambayo ni wateja wa kampuni yao

Pia, ameiomba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuongeza kasi ya kutoa namba au vitambulisho vya taifa ili kampuni za simu ziweze kusajili wananchi kwa kuwa wananchi wako tayari kusajili laini zao za simu za mkononi kwa alama ya vidole kwa kuwa wanaogopa kufungiwa laini zao ifikapo tarehe 31 Desemba mwishoni mwa mwaka huu

Naye Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula ameziomba kampuni za simu za mkononi kuwa sehemu ya kupiga vita maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na kutoa tahadhari kwa wateja wake kupitia ujumbe kwenye simu zao. Pia, ametoa rai kwa wananchi wote nchini kujitokeza kusajili laini zao za simu za mkononi na wasisubiri mpaka siku za mwisho kusajili bali wajisajili kwa wakati ili kuepusha usumbufu na changamoto siku za mwisho

Mabula amewaomba NIDA kuongeza watumishi wa kutosha kutoa vitambulisho vya taifa na amewaomba wabunge wenzake kuhamasisha wananchi na kuwaelimisha kusajili laini zao kwa alama za vidole kwa kuwa tukiwasiliana tunachangia uchumi wa taifa letu ili kufikia uchumi wa kati