Kenya yamaliza nafasi ya pili katika mashindano ya mabingwa wa riadha duniani


Kenya imemaliza nafasi ya pili katika msimamo wa medali wa mashindano ya IAAF ya mabingwa wa riadha duniani yaliyoanza Septemba 27 na kumalizika jana Oktoba 6 mwaka huu huko Doha, Qatar.

Kenya imemaliza mashindano hayo ikiwa na jumla ya medali 11, 5 za dhahabu, 2 za fedha na 4 za shaba. Nafasi ya kwanza imetwaliwa na Marekani huku China ikiondoka katika nafasi ya nne.

Katika hatua ya fainali ya michuano hiyo iliyowakusanya wakimbiaji bora zaidi duniani, Timothy Cheruiyot wa Kenya ameshuhudia akishinda taji la dunia la mbio za wanaume mita 1,500, akiongoza kutoka mwanzo hadi mwisho na kutumia dakika 3 sekunde 29 na nukta 26.

Naye Mganda Joshua Cheptegei pia akiondoka kifua mbele na kushinda mbio za wanaume mita 10,000 akitumia muda mzuri kabisa katika historia ya michezo hiyo wa dakika 26 sekunde 48 na nukta 36. Mkimbiaji huyo mwenye miaka 23 ambaye mwaka 2017 alipata medali ya fedha ni Mganda wa kwanza kushinda taji hilo.