Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma
Serikali imesema itahakikisha inaweka mazingira mazuri ya kuboresha hali ya lishe hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kubeba kikamilifu agenda ya lishe ili kuondoa na kutokomeza madhara yote yatokanayo na utapiamlo na lishe iliyopitiliza.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji) Dorothy Mwaluko, alipokuwa akimuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge kazi, Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu) Jenista Mhagama, wakati wa kufunga mkutano wa 6, wa wadau wa lishe wa kutathmini hali ya lishe hapa nchini na kuweka mikakati mipya ya kuboresha lishe.
Amesema serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha inaboresha hali ya lishe hapa nchini huku, akiwataka watendaji kuhakikisha wanatumia tafiti kufahamu visababishi vya utapiamlo unaotukabili hapa nchini.
"Niwatake watendaji mtumie tafiti za viashiria vya utapiamlo na kupanga mipango ya lishe inayoendana na mazingira yetu kwa kuwa changamoto za lishe zinatofautiana kutoka eneo moja na lingine na wasiwe na mkakati mmoja wa kudhibiti utapiamlo" amesema.
Aidha amesisitiza matumizi ya Sanaa mbalimbali katika maeneo tofauti hapa nchi kutoa elimu ya lishe, kwa kuwa Sanaa ina nguvu hivyo itasaidia katika kutoa elimu ya lishe na kuhakikisha tatizo la lishe duni linakomeshwa.
Amesema wataalamu ni lazima kuhakikisha kaya zinashirikishwa kikamilifu katika vita hii ya kutokomeza utapiamlo kaya zipewe elimu ya kutosha kuhusu madhara ya lishe duni, na kuelimishwa namna ya namna ya kufuata lishe bora.
Amewataka wataalamu kuwekeza katika kutoa elimu ya lishe kwa makundi ya Wazee na vijana barehe kwani ndiko kwenye madhara makubwa na ndio waathirika wakubwa wa kukosa lishe bora.
Amewataka kutumia tathmini na mapendekezo waliyofikia katika mkutano huo wa siku mbili huo kwenda kuboresha maeneo ambayo hayakufanyiwa vizuri katika mpango uliopita wa kuboresha hali ya lishe hapa nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt Zainabu Chaula, amesema tatizo la lishe duni hapa nchini halikutakiwa kuwa tatizo kwani tunachakula cha kutosha, shida ni namna ya ulaji wa chakula hicho.
Amesema yeye kama mtendaji Mkuu wa Wizara hiyo atahakikisha ajenda ya lishe inaingia katika ujumbe wa mbio za Mwenge mwaka mwaka 2020, ili kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia watanzania kwa kiasi kikubwa.
"Mimi kama mtendaji Mkuu wa Wizara hii nitahakikisha ajenda ya lishe naipeleka kwa wakati na inaingia katika ujumbe wa mbio za Mwenge kuhakikisha elimu hii inasambaa kwa kiasi kikubwa katika jamii"
"Pia niwasisitize maeneo yote ambayo kwa mwaka uliopita hamkufanya vizuri mkahakikishe mnaanza nayo na miwekeze nguvu nyingi kuhakikisha mnafanikisha" amesema Dkt Zainabu.
