Na Muhadhi Mohammed,Ruvuma
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme,amesema kuwa kufungwa kwa Benki ya wananchi ya Mbinga mkoani humo kumeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa wakulima na wananchi kwa ujumla.
Mndeme aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha kamati ya ushauri ya maendeleo ya mkoa wa Ruvuma(RCC)katika ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Songea.
Alifafanua kuwa kufungwa kwa Benki hiyo kumesababisha baadhi ya wakulima wilayani humo kushindwa kumudu gharama za uendeshaji wa shughuli za kilimo kutokana na kukosa mikopo mbalimbali ya pembejeo za kilimo iliyokuwa ikitolewa na benki hiyo.
Alisema kuwa katika kukabiliana na hilo,tayari serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wale wote waliohusika katika kuifirisi benki hiyo ikiwa pamoja na kuikabidhi taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU)mkoani humo kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi.
Aidha mkuu huyo wa mkoa alitumia kikao hicho katika kuwahimiza wataalam kuzitumia mvua zilizoanza kunyesha mkoani humo kwa ajili ya kwenda kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima vijijini badala ya kukaa ofisini.
Hata hivyo ametoa onyo kwa mawakala mkoani humo ambao watauza pembejeo za kilimo kwa bei kubwa tofauti na bei elekezi ya serikali kwa madai kwamba yeyote atakayekwenda kinyume na hapo atachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani humo Julius Mtatiro,akichangia hoja katika kikao hicho alisema kuwa hali ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji inazidi kuongezeka hivyo ameshauri kujengwa kwa majosho na kutengwa kwa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya kubaini maeneo ya kilimo na marisho.