Kasi ndogo ya ukusanyaji mapato ya Kodi ya pango la ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Gairo mkoa wa Morogoro imemsononesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ta Makazi Dkt Angeline Mabula na kuagiza halmashauri hiyo kuongeza kasi ili kufikia lengo la mapato ya kodi ya ardhi.
Akiwa katika ziara yake ya siku moja katika wilaya hiyo jana tarehe 19 Novemba 2019 Dkt Mabula alielezwa na Afisa Ardhi katika halmashauri ya Gairo Nicolaus Matsuva kuwa halmashauri hiyo katika kipindi cha mwaka 2018/2019 imekusanya shilingi milioni 12.3 na mwaka huu kufikia Novemba imekusanya milioni 10 ya kiwango ilichopangiwa cha milioni 55.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, kiwango hicho cha makusanyo katika halmashauri ya Gairo ni kidogo na hakijafikia hata nusu ya makadirio ya shilingi milioni 55 iliyowekewa halmashauri hiyo kukusanya kwa mwaka na makadirio hayo hayalingani na uhalisia wa makusanyo ya halmashauri.
Aliitaka halmashauri ya Gairo kupitia idara yake ya ardhi kuongeza kasi ya makusanyo ya maduhuli ya kodi ya pango la ardhi kwa kuwa kodi hiyo ndiyo inayoisaidia serikali kutekeleza miradi mikubwa aliyoieleza kuwa mingi inataegemea kodi ya ndani. ‘’Msipokusanya kodi ya ardhi mjue mnamkwamisha Mhe Rais kutekeza miradi mikubwa kama vile mradi wa kufufua umeme wa Mwl. Nyerere maarufu kama stiglers hivyo ni lazima tuongeze kasi ya makusanyao’’ alisema Dkt Mabula.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Sirieli Mchembe alisema, wilaya yake ina changamoto kubwa ya ujenzi holela na kubainisha kuwa hata zoezi la urasimishaji katika wilaya hiyo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo sebule za baadhi ya nyumba kuelekezwa kwenye vyoo vya nyumba nyingine.
Hata hivyo, alimuahidi Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa ofisi yake itayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa.
Katika hatua nyengine Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alitembelea hifadhi ya Msitu wa Ukaguru uliopo Tarafa ya Nongwe kata ya Mandege wilaya ya Gairo mkoa wa Morogoro na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu.
