Wakulima wa korosho Ruangwa, Liwale na Nachingwea wakumbushwa jambo


Na Ahmad Mmow-Nachingwea

Wakulima wa korosho waliopo katika wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Liwale wamekumbushwa kuhakiki akaunti zao kabla ya kuingiziwa malipo yao.

Wito huo ulitolewa jana mjini Nachingwea na Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha RUNALI, Hassan Mpako alipozungumza na Muungwana Blog alisema miongoni mwa sababu zinazosababisha baadhi ya wakulima kuchelewa kupata malipo yao kw awakati ni kushindwa kutoa fedha zao kwenye akaunti kutokana na akaunti hizo kulala.

Alisema ili kuepuka hali hiyo inayosababisha malalamiko ni wakulima kuangalia akaunti zao kabla ya kupeleka korosho zao maghalani kwa ajili ya mauzo.

''Kwa kufanya hivyo watakuwa wanajua kama akaunti zao zinafanyakazi au hazifanyikazi. Sababu baadhi ya wakulima akaunti zao zinakuwa zimelala na wanashindwa kutoa fedha, mwisho wa siku wanalalamika,'' Mpako alisema.

Mbali na kutoa wito huo kwa wakulima, Mpako amewataka makatibu wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) wazingatie na kufanyia kazi maelekezo wanayopewa na maofisa wa benki hasa kufanyia marekebisho kasoro zinazojitokeza kwenye taarifa hao.

Alisema licha ya chama hicho juzi kupokea gunia 90,000, lakini pia kinatarajia kupokea gunia 220,000 ndani ya juma hili, ambazo nazo zitasambazwa kwenye AMCOS zinazounda chama kikuu hicho.