China kujenga hospitali kutibu wagonjwa wa Corona

China inaharakisha ujenzi wa hospitali mpya ndani ya muda wa siku 10 ili kuwatibu wagonjwa wa kirusi hatari cha Corona ambacho tayari kimeshasambaa kwa mamia ya watu.

Hospitali hiyo inayojengwa kwenye mji wa Wuhan, ambako soko lake la samaki ndilo kitovu cha mripuko wa kirusi hicho, inatarajiwa kuwa tayari ifikapo Februari 3 kuhudumia idadi ya wagonjwa inayoongezeka.

Tayari watu 830 wameshaambukizwa kirusi hicho, huku 26 wakipoteza maisha na mamilioni wengine wamewekwa chini ya karantini katika juhudi za kujaribu kudhibiti kusambaa kwake.

Wakati huo huo, safari za ndege kati ya mji wa Moscow na Wuhan zimesitishwa kutokana na wasiwasi wa kuenea kwa virusi vya Corona.

Hayo yanajiri wakati taasisi inayoshughulikia chanjo na kinga za maradhi duniani imesema, chanjo dhidi ya kirusi hicho inaweza kupatikana katika kipindi cha mwaka mmoja unaokuja.
Mpya zaidi Nzee zaidi