Mchemo B wachangamkia hati za kimila za kumiliki ardhi.



Na Ahmad Mmow, Newala.

Wananchi 15 kati ya 70  wakazi wa kijiji cha Mchemo B, wilaya ya Newala, mkoa wa Mtwara ambao waliomba hati za kimila ili wamiliki mashamba yao( ardhi) ili waepuke migogoro inayojitokeza mara kwa mara ya kugombea ardhi.

Hayo yameelezwa na mtendaji wa kijiji cha Mchemo B, Ashura Idd Mohamed, alipozungumza na Muungwana Blog kijijni hapo baada ya kuombwa aeleze ni migogoro gani ya kijamii inayotokea mara nyingi na mchango wa kituo cha msaada wa kisheria na haki za binadamu wilayani Newala( PCO) katika kutatua na kusuluhisha migogoro.

Ashura alisema wananchi hao 15 waliopata hati za kimila ni kati ya 70 walioomba hati za kimila baada ya kukamilisha masharti na vigezo. Huku wengine wakishindwa kukamilisha na kutekeleza vigezo hivyo ili wapate hati hizo.

Alisema kikwazo kikubwa kinachosababisha baadhi ya waombaji hao kushindwa kukamilisha na kutekeleza vigezo hivyo ni kushindwa kumudu gharama za upimaji maeneo yao. Hali inayosababisha wakusanye nguvu ili wakamilishe masharti na vigezo hivyo.

Alisema uchangamkiaji huo wa hati za kimila umetokana na uhamasishaji uliotolewa na viongozi wa kijiji hicho kutokana na migogoro ya ardhi iliyokuwa inajitokeza. Kwani baadhi ya wananchi walifikia hatua ya kupora maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kijamii na umma.

" Watu wanahitaji kupata hati za kimila, lakini tatizo ni uwezo wa kumudu gharama za upimaji. Kwani wengi baada ya kupata elimu wanajua umuhimu wa kupata hati hizo,'' alisema Ashura.

Kuhusu mchango wa PCO katika kusuluhisha na kutatua migoro, Ashura alisema kituo hicho ni msaada mkubwa kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kuweka wanasheria wa kuwatetea. Kwahiyo kimbilio lao ni kwenye vituo na mashirika ya msaada wa kisheria.

Kwaupande wake mratibu wa PCO, Juma Mnali alisema kunaumuhimu mkubwa wa wananchi kupewa elimu ili wajue faida ya kuwa na hati hizo. Hata hivyo kunahaja ya kuangalia upya njia itayowawezesha wananchi wenye vipato vidogo waweze kumudu gharama.

" Nadhani kunahaja ya kulipa kwa awamu gharama za upimaji. Watu walipe kidogokidogo hadi watakapomaliza ndipo wapimiwe na kupewa hati hizo za kimila," alisema Mnali.

Mratibu huyo wa PCO alisema kwakuwa huwa wanakutana na ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Newala,  watafikisha wazo hilo ili lipelekwe kwenye baraza la madiwani.