https://monetag.com/?ref_id=TTIb Serikali yaanza kukarabati miundombinu chuo FDC Masasi | Muungwana BLOG

Serikali yaanza kukarabati miundombinu chuo FDC Masasi

Na Hamisi Abdulrahmani, Masasi

  UONGOZI wa Chuo Cha Maendeleo ya wananchi wilayani Masasi mkoani Mtwara(FDC) umeishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha sh.milioni 570.1 kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Chuo hicho ikiwemo kujenga majengo mengine mapya sita.

   Awali Chuo hicho kilikuwa kikikabiliwa na tatizo la uchakavu wa majengo yake hasa mabweni ya wanafunzi pamoja na madarasa hali iliyowasukuma uongozi kuiomba Serikali juu ya utatuzi wa changamoto hiyo.

  Pongezi hizo zilitolewa jana wilayani Masasi na Mkuu wa Chuo hicho,kwa niaba ya uongozi wa Chuo hicho,Alfani Mshana alipokuwa akizungumza waandishi wa habari ofisi kwake juu ya changamoto zilizopo katika Chuo hicho.

  Mshana alisema tarayi wameshapokea fedha hizo zilizotolewa na Serikali kiasi cha sh.milioni 570.1 kwa ajili ya ukarabati huo wa majengo ambayo yalikuwa ni chakavu.

  Alisema ukarabati wa majengo pamoja na ujenzi wa majengo mapya sita katika Chuo hicho tayari umeshaanza na baadhi ya majengo ukarabati wake unatarajia kukamalika hivi karibuni.

  "Tunamshukuru sana raisi Dk.John Pombe Magufuli kwa kutupatia fedha hizi sh.milioni 570.1 ili tuweze kukatabati majengo ya Chuo hiki ikiwemo kujenga majengo mengine mapya ikiwemo bweni la wanafunzi," alisema Mshana 

  Alisema Chuo hicho kina zaidi ya wanafunzi wapatao 300 ambao ni wasichana na wavulana hivyo uboreshaji huo unaofanywa na serikali utasaidia kukipa hadhi chuo hicho cha wananchi Masasi.

  Aidha,Mchana alisema bado jamii hasa kwa mikoa ya kusini haijawa na mwamko chanya wa kutambua thamani ya uwepo wa Chuo hicho hivyo hata hamasa ya kuwapeleka watoto wao kusoma hapo bado ni ndogo.

  Alisema Chuo hicho kinatoa fani mbalimbali kwa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo ikiwemo stadi za maisha, ushonaji, uwashi, mapishi,utengenezaji wa magari, umeme wa majumbani na magari.

  Mshana alisema kupitia fani hizo zinazotolewa shuleni hapo tayari Chuo hicho kimeshazalisha wanafunzi wengi nchini ambao kwa sasa wamejiajiri na baadhi wameajiliwa katika sekta za umma pamoja na Serikalini.

  " Licha ya Serikali kutupatia fedha hizi kwa ajili ya changamoto hii ya uchakavu wa majengo lakini changamoto nyingine tuliyonayo hapa ni upungufu wa walimu tuna walimua saba wakati mahitaji ni zaidi ya hapo, "alisema Mshana

  Kwa upande wake mmoja wa mwalimu wa Chuo hicho,Maliki Liyanga alisema wanaishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo za ukarabati wa majengo.