Tume ya maridhiano yabaini makaburi ya pamoja Burundi

Makaburi 4,163 ya pamoja yamepatikana nchini Burundi kufuatia uchunguzi wa mwaka mmoja, imesema tume ya ukweli na maridhiano.

Tume hiyo iliyopewa jukumu la kubaini ukweli katika nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo wa kikabila tangu ilipopata uhuru, imesema kuwa imepata majina ya watu 142,505 waliouawa tangu mwaka 1962 ya uhuru.

Katika baadhi ya mikoa 18 ya nchi hiyo kumegunduliwa mamia ya makaburi ya pamoja.

Makaburi 640 yalipatikana katika eneo la Gitega ambalo ni makao makuu mapya ya serikali, inasema ripoti hiyo ilitolewa na tume hiyo leo Jumanne.

Siku ya Jumatatu tume hiyo iliweka wazi kwa umma kaburi la pamoja lililopatika viungani mwa mji wa Bujumbura ambako mabaki ya miili ya watu kati ya 250 na 270 ilipatikana.

Watu hao wnasadikiwa kuuawa na wakati wa makabiliano kati ya majeshi ya jamii ya Watutsi-waliokuwa wengi na kundi la waasi wa Kihutu kufuatia mauaji ya rais Melchior Ndadaye mwaka 1993, Tume hiyo ilisema.

"Makaburi mengi zaidi yanatarajiwa kupatikana kwasababu watu wanayajua lakini wanaogopa kuzungumza au walipata usumbufu wa kiakilia" - Pierre-Claver Ndayicariye , mwenyekiti wa tume hiyo alisema wakati wa kuwasilisha ripoti hiyo kwa bunge leo Jumanne.

Baada ya kuonesha makaburi ya pamoja ya Bujumbura, Naibu mwenyekiti wa tume hiyo Noah Clément Ninziza aliambia BBC kwamba "Baadhi ya watu wamewatambua jamaa zao katika mabaki hayo; watu walikuwa wakilia, walishangaa,"

Baada ya kupata uhuru mwaka 1962 Burundi ilikabiliwa na mzozo wa kikabila kati ya Wahutu na Watutsi uliochochewa kisiasa, mauaji yalifanyika miaka ya 1965, 1969, 1972, 1988 na 1993.

Bw. Ndayicariye alisema kupata ukweli kuhusu kile kilichofanyika kutasidia kuleta maridhiano kati ya waliotekeleza mauaji na waathiriwa wa mauaji hayo ili "kufikia amani ya kudumu nchini Burundi kwa vizazi vijavyo".