Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Zanzibar itaendelea kupata umaarufu katika maeneo mbali mbali Duniani kupitia Muziki wake wa Taarab ambao umekuwa na mvuto wa kipekee hasa kwa wale wanaoamua kuufuatilia ili kujiburudisha.
Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} kilichopo Mtaa wa Mizingani pembezoni mwa Fukwe ya Forodhan alipokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezishauri na kuziomba Taasisi na Washirika wa Maendeleo kukiunga mkono Chuo hicho wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiangalia mazingira na kutafuta mbinu zitakazosaidia kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokikabili Chuo hicho.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} Bibi Alessia Lombardo amesema Wahitimu wapatao 170 humaliza Mafunzo yao Kila Mwaka tokea kilipoanzishwa Chuo hicho Mnamo Mwaka 2002 kikiwa na Miaka 18 sasa.
Nao kwa upande wao Mwalimu Mkuu wa Chuo hicho Mohamed Othman pamoja na Wakufunzi wenzake Kassim Ali Basalamu na Hassan Mahenge wamesema kuwa mbali ya jukumu lao chuoni hapo lakini pia hutenga muda wa kutoa Mafunzo kwa Wanafunzi wenye mahitaji Maalum katka Skuli ya Msingi ya Kisiwandui.


