Ujerumani: Mshukiwa wa shambulio la carnival akamatwa

Waendesha mashtaka nchini Ujerumani wamesema jana kwamba kijana mwenye umri wa miaka 29 aliyejeruhi zaidi ya watu 61 mjini Volkmarsen amekamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuua na kusababisha madhara mabaya ya mwili kwa binadamu bila ya kujali.

Kijana huyo ndiye mshukiwa pekee katika shambulio hilo dhidi ya watu waliokuwa wakisherehekea tamasha la kitamaduni carnival.

Wengi miongoni mwa majeruhi walikuwa ni watoto. Polisi imesema mshukiwa huyo alijaribu kwa makusudi kuvamia umati wa watu akiwa ndani ya gari kwa nia ya kuwaua.

Imeongeza kwamba imeshindwa kumhoji rasmi mtuhumiwa mkuu kutokana na kiwango cha majeraha aliyoyapata wakati wa shambulio hilo.

Hadi sasa hakuna ushahidi wowote wa kuashiria kwamba shambulio hilo lilichochewa na misimamo ya kisiasa.