Urusi yakataa kusitisha mapigano Idlib

Urusi imetangaza jana kwamba haitokubaliana na makundi ya waasi inayoyazingatia kuwa ni ya kigaidi kusitisha mapigano katika mkoa wa Syria wa Idlib.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergey Lavrov amesema mapatano yatawahamasisha kuendelea kukiuka sheria za kimataifa.

Raia wa kawaida wapatao 19 wameuawa Idlib hapo jana, kulingana na Shirika la Kusimamia Haki za Binadamu Syria. Miongoni mwao ni watoto wanane waliouliwa na mashambulizi ya anga ya vikosi vya serikali.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imezitolea wito pande zinazopigana kuruhusu njia salama ya raia wa kawaida kukimbia mashambulizi hayo.

Vurugu za mkoa wa Idlib zimesababisha idadi kubwa ya watu kupoteza makazi yao katika historia ya dunia ya miaka ya hivi karbuni pamoja na idadi kubwa ya vifo.