DC Komba awaonya viongozi wa soko kuu la Nachingwea



Na Ahmad Mmow, Nachingwea.

Mkuu wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Hashim Komba amesema hatasita kuwachukulia hatua kali viongozi wa  soko kuu la Nachingwea ambao watabainika kutumia vibaya fedha zinakusanywa kutoka kwa wafanyabiashara wanaofanyia biashara kwenye soko hilo. ¥ Komba ametoa onyo hilo leo alipozungumza na wafanyabiashara na viongozi wa soko kuu la Nachingwea akiwa sokoni hapo.

Komba alisema kumekuwa na malalamiko na malumbano ya mara kwa mara ambayo mengine yanahusu matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa kutoka kwa wafanyabiashara. Kwahiyo hayupo tayari kuona hali hiyo inaendelea.

Alisema viongozi hawanabudi wawe waadilifu na waaminifu badala ya kuhujumu jitihada za wafanyabiashara ambao licha ya ugumu wa biashara wanajitahidi kutoa michango na ushuru. Hivyo hatasita kuwachulia hatua kali wataobainika kutumia vibaya mapato yanayotokana na soko hilo.

Katika kile kilichoonesha alikuwa hatanii kutoa onyo hilo, Komba amewataka viongozi waliomaliza muda wao wakabidhi taarifa zote kwa viongozi wapya. Ikiwamo taarifa za mapato na matumizi, hadi jumatano ya wiki ijayo wawe wamekabidhi taarifa hizo. Huku akiwataka wapelekee taarifa ya salio la fedha zilizopo benki.

 '' Niletewe bank stetment ili nijue watakuwa wamekabidhi shilingi kwa viongozi waliopo,'' alisisitiza Komba.

Aidha mkuu huyo wa wilaya amewataka viongozi wa soko waitishe mkutano ili wafanyie marekebisho katiba ya umoja wa wafanyabiashara. Kwani katiba iliyopo inamapungufu yanayohitaji marekebisho.

Aliyataja baadhi ya mapungufu hayo kuwa nikutokuwepo haki kwa wanachama kukata rufaa kupinga maamuzi mbalimbali. Ikiwamo kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi wa viongozi wa wafanyabiashara hao.

Mbali  hayo, Komba amewataka viongozi wa soko hilo waandae na wajenge eneo la maegesho ya vyombo vya usafiri vya wafanyabiashara na wanunuzi katika soko hilo. Hasa pikipiki na baiskeli. Huku mwenyewe akihaidi kuchangia mifuko mitano ya saruji kwa ajili ya ujenzi huo.