Shirika la Interpol linasema uhalifu umeongezeka pakubwa katika kipindi hiki cha mripuko wa virusi vya corona wakati ambapo wahalifu na magenge wanaboresha mbinu zao kwa haraka.
Katika ripoti iliyochapishwa mjini The Hague hii leo wachunguzi wamegundua kwamba kuna ongezeko la visa vya uhalifu wa kimtandao, ulaghai, wizi na kughushi stakabadhi.
Ripoti hiyo inasema uuzaji wa bidhaa ghushi za kujikinga na virusi vya corona ikiwemo barakoa, dawa za maji za kuua vijidudu na dawa zengine umeongezeka tangu mzozo huu ulipoanza.
Mwezi huu wa Machi barakoa ghushi 34,000 zilikamatwa katika operesheni ya polisi iliyofanywa kote duniani. Dawa ghushi ambazo zimepatikana kusambazwa ni dawa za kupambana na virusi, dawa ya kukabiliana na malaria ya chloroquine na dawa zengine za vitamini.
Mkurugenzi wa Europol Catherine De Bolle amesema jambo hili halikubaliki.
