Kanisa kugawa barakoa za vitambaa kwa waumini

PAROKIA ya Mt. Vicent wa Paulo Katubuka Jimbo la Kigoma imeweka mkakati wa kuhakikisha kila muumini pamoja na familia yake kila mmoja anapata barakoa mbili za kufua kama hatua ya kuwezesha kujikinga na ugonjwa wa  virusi vya corona.

Paroko wa parokia hiyo, Padre Stephene Shaiju, ndiye aliyeeleza mikakati hiyo leo Aprili 26 wakati wa misa takatifu iliyoazimishwa parokiani hapo iliyoambatana na utolewaji wa elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.

Amesema wameamua kuweka mkakati wa kuunganisha nguvu zao pamoja ili kuwawezesha waumini  na familia zao kujikinga pindi wanapokuwa kanisani na sehemu zingine.

Padre Shaiju, amesema kwa uhalisia vipato vya walio wengi hawawezi kumudu gharama za manunuzi ya barakoa hivyo mpango huo utawezesha mwenye uwezo kutoa fedha ,vifaa kama Cherehani za kushonea na wenye ujuzi wa kushona pia kujitolea kufanya kazi hiyo na baadae vifaa kinga hivyo vitagawiwa kwa waumini wote.

‘’Inabidi tuunganishe nguvu kwa pamoja katika hili ili kusaidiana, mwenye Cherehani ailete, mwenye uwezo wa kununua vitambaa alete na Masisita wetu watatuelekeza namna ya kushona barakoa, lakini pia daktari atatuelekeza kitambaa sahihi kinachokidhi vigezo" amesema.

Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Kabanga iliyopo wilayani Kasuku Dk. Peter Mayengo akitoa maelekezo ya kitalamu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo wakati wa misa hiyo, amesema wananchi wanapaswa kutopuuza maelekezo yanayotolewa na Serikali kupitia watalamu mbalimbali wa afya.

Daktari Mayengo amebainisha baadhi ya mambo muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuyazingatia kuwa ni kuacha mikusanyiko isiyo ya lazima, kutumia barakoa, kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka kwa sekunde zisizopingua 20 kutojigusa katika maeneo ya uso ambayo watalamu wanashauri kama macho na pua.

Mmoja wa waumini katika Parokia hiyo, Sesilia Ntilampa amesema wazo la kuunganisha nguvu kwa pamoja kusaidiana katika jambo hilo nilakupongezwa na nimsaada kwa wasio na uwezo wa kumudu gharama za kununua vifaa kinga hivyo.

 Askofu wa Jimbo Katoriki Kigoma, Askofu Joseph Mlola ametoa wito kwa wazazi kuongeza ulinzi kwa watoto wao katika kipindi hiki ambacho hawaendi shule kwani baadhi yao wamekuwa wakirandaranda mitaani jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
Mpya zaidi Nzee zaidi