Na Rebeca Duwe, Tanga.
Chama Cha wananchi (CUF) kimewataka wanachama wake wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi Mkuu ujao kuanza maandalizi mapema ikiwemo kutia nia .
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba wakati akizungumza kwenye mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi ili kuweza kuwapa moyo wale wenye nia na uthubutu.
Profesa Lipumba aliwataka wenye uthubutu wa kugombea nafasi za Udiwani,Ubunge na Urais wasione hofu kuwania nafasi hizo bali waanze maandalizi mapema ili pale kipenga kikitangazwa wawe wapo tayari.
"Nafasi za siasa zinahitaji maandalizi hivyo niwatake wanachama wangu wenye Nia ya kuwatumika wananchi wa nchi hii Basi waanze kujitayarisha kwa ajili ya kugombea "alisisitiza Profesa Lipumba.
Aidha alisema kuwa swala la kutia Nia tafsiri yake ni kuchukuwa fomu,kujaza na kurejesha Kisha kusubiri mchujo wa kura za maoni ambapo swala hilo haliwezi kuathiriwa na uwepo wa ugonjwa wa Corona.
Vile vile Mwenyekiti huyo aliwahamasisha wanawake wenye uwezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwa ajili ya kuwatumika wananchi badala ya kurudi nyuma kwa kujihofua uwezo wao.
"Wanawake ni miongoni mwa viongozi Bora lakini kinachowashinda ni uwoga wao lakini niwatake watumie mafanikio ya wanawake wenzao waliothubutu Kama chachu ya wao nao kugombea"alisema Lipumba.
"Ninavyoona Mimi changamoto iliyokuwepo ni kuitisha vikao vya kura za maoni katika kipindi hiki Cha uwepo wa ugonjwa wa covid19 kwani wataalamu wa Afya wametushauri kuepuka mikusanyiko "alisema .
Aidha Mwenyekiti Lipumba alisema kuwa watahakikisha wanasimamia sera ya Chama hicho ya haki sawa na furaha kwa wote .
Hata hivyo akizungumza athari za ugonjwa wa corona katika shughuli za kichama ,Prof.Lipumba alisema kuwa chama kimezuia shughuli za uimarishaji wa Chama kwa sasa katika ngazi zote za wilaya,Majimbo na Kata .
