Na Thabit Madai,Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyeki wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) awamu ya saba ya imefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa ugonjwa virusi vya corona ikilinganisha hali ilivyokuwa awali.
Dk Shein ametoa kauli hiyo hapo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa maabara ya kisasa pamoja na eneo litakaloanza ujenzi wa Hospitali ya kubwa ya kisasa ya Binguni Mkoa wa Kusini Unguja.
Dk Shein alisema kwamba hali ya maradhi ya virusi vya corona kwa sasa nchini imedhibitiwa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali.
Alisema hali hiyo imetokana na Serikali yake ya awamu ya Saba kufanya jitihada kubwa katika kudhibiti maradhi hayo na kutowaathiri wananchi.
“Juzi nilisema Pemba na hapa nataka kuwaambia kuwa hali ya Corona tumeidhibiti kwa kiasi kikubwa sivyo tulivyotarajia, hali mwanzo ilikuwa mbaya wenzetu bado wanateseka na maradhi haya,” alisema Dk Shein.
Aidha Dk Shein Alieleza kuwa Serikali hapo awali ilitoa maelekezo ya mambo 10 kwa wananchi ikiwemo kufungwa skuli, vyuo vikuu, madrasa na mambo mengine lakini hali ikiendelea hivyo basi na serikali itatoa tamko kuruhusu shughuli mbalimbali ziendelee kama alivyosema Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
“Tunaendelea kuangalia hali ya maradhi yanavyokwenda na itakapofika wakati na sisi tutasema skuli zinafunguliwa lini na mambo mengine,” alisema.
Alisisitiza kuwa, serikali haijakubaliana na watu wanaotaka kufungwa mipaka kwa ajili ya korona na kubainisha kuwa serikali inataratibu zake na mipango yake.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekataa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imekataa hivi tunavyokwenda sisi ndio utaratibu wetu na tunakwenda vizuri,” alisema.
Sambamba na hayo, Rais Shein, alisema serikali haikatai kushauriwa bali ni busara kwa watu wanaotaka kushauri kupitia njia sahihi kuliko kusema milango ya nyuma.
“Wao serikali hawataki kuitambua na hata mimi hawanitambui sasa wanamwambia nani serikali isisafirishe boti zisimame na maneno mengine,” alisema.
Dk. Shein, alisema hashindani na mtu yoyote kwani yeye ni kiongozi na ana majukumu makubwa kwa wananchi wa Zanzibar na hayupo tayari kushindana na mtu yoyote.
Akizungumzia ziara hiyo Dk Shein alisema kuwa Serikali itaanza maanalizi ya ujenzi wa Hospitali ya Binguni kwa pesa zake wenyewe ikiwemo ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura na watu wanaopata Ajali.
Alisema pamojana serikali kutokuwa na pesa za kujenga majengo yote katika hospitali hiyo lakini tayari imeshapata pesa za mkopo na wakati wowote zitaingizwa Serikalini.
Aidha, alisema kazi iliyopo hivi sasa ni kuona eneo lote linasafishwa na kuanza kupimwa ili kuona ujenzi huo unaanza ikiwemo kuchimbwa misingi.
Dk. Shein, alifahamisha kuwa serikali imedhamiria kuanza kwa kasi ujenzi huo ilikuwa ikisita kutokana na janga la korona lilokumba nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania.
Alisema, ujenzi wa hospitali hiyo utafanywa na kampuni ya ujenzi ya serikali kama kampuni nyengine.
Alisema majengo yote yakishakamilika katika hospitali hiyo basi kijiji cha Binguni kitabadilika kimazingira.
“Haya yote tunaamua Baraza la Mapinduzi kama tulivyoamua mambo mengine ikiwemo kununua Mv. Mapinduzi 11, Meli ya Mt. Ukombozi na majengo ya kisasa ikiwemo shopping moll basi na majengo haya tumekubaliana tuanze ujenzi na watakaokuja wataendeleza", alisema.
Akizungumzia maabara ya kisasa katika eneo hilo Rais Shein, ameagiza wataalamu kukaa pamoja na kukubaliana katika ujenzi huo na wakati wowote kuanzia mwezi huu mafundi wataanza ujenzi huo na kuona unakamilika kama ilivyotarajiwa ndani ya miezi mitatu.
Hata hivyo, alisema machine zilizotolewa na mzalendo rostam Aziz kwa ajili ya uchunguzi wa korona haitafungwa katika maabara hiyo na badala yake itapelekwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja au hospitali ya Wete kisiwani Pemba.
"Hapa tutaweka machine ngengine sio lazima ile ianze kazi za uchunguzi hapa lakini jengo hili ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar uchunguzi na utafiti utafanywa hapa" alisema.
Nae, Waziri wa Nchi Ofisini ya Rais Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir, alisema kazi inayoanza katika ujenzi wa hospitali ya Binguni ni kuazima vifaa katika wizara ya ujenzi mawasiliano na usafirishaji ili kuanza kusafisha eneo hilo.
Hata hivyo, alimhakikishia Dk. Shein mpaka sasa ukiachia wananchi wa awali waliovamia katika maeneo hayo na kujenga nyumba za makaazi hakuna wengine walioingia katika eneo hilo.


