Kanisa kuu la madhehebu ya Katoliki duniani, la Mtakatifu Petro lililoko Vatican limefunguliwa leo Jumatatu kwa ajili ya wageni baada ya kufungwa kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na sheria iliyotangazwa Italia ya vizuizi kwa lengo la kudhibiti kusambaa kirusi cha corona nchini humo.
Wageni wachache walipanga foleni leo wakizingatia amri ya watu kutosogeleana karibu, na kupimwa joto kabla ya kuingia ndani ya kanisa hilo huku polisi wakilinda. Kanisa hilo lilifungwa tangu tarehe 10 mwezi Machi.
Na Italia ilikuwa nchi ya kwanza kufunga shughuli zote nchi nzima kwa zaidi ya miezi miwili iliyopita na kuufanya uchumi wa taifa hilo kuporomoka. Kufikia sasa idadi rasmi ya waliokufa kutokana na kirusi hicho nchini humo ni kiasi watu 32,000.
Makanisa yote mjini Rome yalifungwa mwanzoni mwa mwezi Machi.