China yatangaza hatua mpya dhidi ya vyombo vya habari vya Marekani

China imeyataka mashirika manne ya habari ya Marekani kutoa maelezo ya kina kuhusu operesheni zao nchini China ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi katika ugomvi wa vyombo vya habari na utawala wa Trump.

Mashirika hayo ya Associated Press, United Press International, CBS News na National Public Radio yanahitajika kufichua taarifa kuhusu wafanyakazi wao, taarifa za kifedha, operesheni zao pamoja na mali isiyohamishika nchini China katika siku saba zijazo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China, Zhao Lijian amesema maelezo hayo ni muhimu ili kukabiliana na hatua ya Marekani ya kuvikandamiza vyombo vya habari vya China nchini Marekani.

Mwezi uliopita Marekani iliamuru kuwa mashirika manne ya habari ya serikali ya China, China Central Televisheni, China News Service, Peoples Daily na Global Times kujisajili kama ujumbe wa kigeni, hivyo kukabiliwa na masharti sawa na ofisi za kibalozi nchini Marekani.

Nchi hizo mbili zimezozana kuhusu operesheni za vyombo vya habari kwa miezi kadhaa, wakati kukiwa pia na mvutano wa mambo ya kibiashara, mlipuko wa virusi vya corona na uhuru wa Hong Kong.