Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu jana ameionya Lebanon na kundi la wanamgambo la Hezbollah kuwa shambulizi lolote dhidi ya nchi yake litajibiwa vikali .
Matamshi ya Netanyahu yamekuja saa chache tangu Israel iliposema kuwa imefanikiwa kuzima jaribio la kuvuka mpaka lililofanywa na watu wenye silaha.
Katika taarifa aliyoitoa akiwa sambamba na waziri wa ulinzi Benny Gantz, Netanyahu amesema kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran litafanya makosa makubwa iwapo litajaribu kutishia usalama wa Israel.
Hapo kabla Jeshi la Israel lilisema kuwa askari wake walifyetua bunduki dhidi ya kundi la wanamgambo wenye silaha waliovuka mpaka na kuingia Israel wakitokea Lebanon.
Wiki iliyopita Israel iliongeza idadi ya wanajeshi kwenye mpaka wake wa kaskazini baada ya kuzidi mvutano na kundi la Hezbollah linaloilamu nchi hiyo kwa mauaji ya mwanamgambo wake mmoja katika shambulizi la anga lililotokea Julai 20 nje kidogo ya mji mkuu wa Syria, Damascus.
