Kanuni sita sita za ufugaji bora wa kuku wa kienyeji


Kuku wa kienyeji ni wazuri kwa ufugaji kwa sababu: Wanavumilia sana magonjwa, Ni
rahisi kuwahudumia, Chakula chao ni cha bei ya chini, Wavumilivu wa hali tofauti za
hewa, Hawahitaji uangalizi wa karibu, na soko lake ni kubwa sana na bei nzuri). 

Hii haimaanishi kwamba, uwaache kuku bila uangalizi, kwani nao hupata magonjwa kama
wasipo patiwa chanjo sahihi, hupungua uzito na uzalishaji mayai hushuka kama wasipo
patiwa chakula chenye virutubisho vyote. Hapa naelezea vitu muhimu katika hii formula
ya ufugaji kuku wa kienyeji kwa mafanikio:

1. Aina ya kuku: Chagua aina ya kuku wenye uwezo wa kutaga mayai mengi na wakati
huohuo, kuzalisha nyama nyingi. Hii itakupa faida kote, kwenye upande wa nyama na
upande wa mayai. Kuku hawa wanajulikana kama Chotara, wanatabia sawa na kuku
wa kienyeji wenye asili ya Tanzania wanaopatikana maeneo mengi nchini; kutokana na
uvumilivu wao wa magonjwa na hali tofauti za mazingira. Pia wanauwezo wa kutaga
mayai mengi (Wastani wa mayai matano kwa wiki) karibu sawa na kuku wa kizungu.
Aina ya kuku hawa ni kama vile, Chotara wekundu (Rhode Island Red), Black
Australorp (Weusi/Malawi), Barred Plymouth Rocks (Madoa), New Hamshire Red,
Kuroila wanapatikana sana Uganda, na Kari kutoka Kenya. Hizi ni aina ya kuku zinazo
patikana Tanzania.

2. Chanjo: Kama nilivyosema mwanzo, kuku wa kienyeji ni wavumilivu wa magonjwa
lakini si kwamba hawayapati, kuna magonjwa ambayo ni hatari pia kwa kuku wa
kienyeji. Chanjo ni muhimu kuwaepusha na hatari ya kuyapata magonjwa haya. Chanjo
muhimu kwa kuku wa kienyeji ni; New Castle, Gumboro, Marek’s na Ndui ya kuku.
Fuata utaratibu wa chanjo kutokana na ushauri wa daktari.

3. Chakula: Kuku wa kienyeji pia wanahitaji mchanganyiko sahihi wa chakula, ili
waweze kukupatia mazao mengi na bora, na kuwaepusha na magonjwa. Zipo fomula
mbalimbali za chakula kutokana na umri wa kuku, na aina ya kuku. Kuku wote
wanahitaji chakula chenye mchanganyiko sahihi wa Madini, Vitamini, Protini, Fats,
Wanga, Vyakula vya kulinda mwili ili usipatwe na maradhi, na Maji safi. Muhimu
kuwapatia kuku majani kama ziada ya chakula, hii hupunguza gharama za chakula na
kuwafanya kuku waonekane wenye afya bora. Ni vizuri kuwapatia vifaranga chakula
spesheli cha dukani kama huna ujuzi wa kutengeneza mwenyewe. Kwani vifaranga
wengi hufa kutokana na kutokupata chakula chenye mchanganyiko sahihi kwao. Kuku
wa mayai pia wanahitaji mchanganyiko sahihi ili waweze kutaga mayai kwa wingi.

4. Banda: Kuku wa kienyeji pia, wanahitaji banda au nyumba ya kuku imara ili kuweza
kuwakinga na baridi kali, wanyama hatari, na wizi. Banda pia liwe na sehemu nzuri za
kutagia na sehemu za kulala ziwe juu , kwani kuku hupendelea kulala juu. Ni muhimu
banda liwe katika hali ya usafi muda wote. Kwa hivyo ni vizuri linyanyuliwe juu kidogo ili
kuruhusu uchafu kuanguka chini na lijengwe ka kutumia mbao, mabanzi, milunda,
nyavu, na mabati. Vifaranga wanahitaji kutenganishwa na kuku wakubwa. Banda si
lazima liwe la gharama kubwa, kwani mafanikio ya ufugaji wa kuku ni vile unavyo
waangalia na si banda. Mada inayohusu mabanda bora ya kuku itakuja hivi karibuni.

5. Majogoo kwa majike: Ili mayai mengi yaweze kutotolewa, ni vizuri jogoo mmoja
aweze kuwahudumia majike wasiozidi 7. Kwani kuku wanaweza kutaga bila ya jogoo,
lakini mayai hayatoweza kuleta kifaranga. Ili mayai yalete vifaranga ni lazima yawe
yamerutubishwa (Fertilized eggs) na jogoo. Kwa hivyo ni vizuri kuweka Jogoo 1 kwa
majike 7, hivyohivyo Jogoo 2 majike 14, Jogoo 3 majike 21, n.k. Pia hakikisha kuku
wanao tumika kuendeleza kizazi ni wale wenye afya bora. 

6. Vyombo vya chakula: Hakikisha vyombo vya chakula ni visafi na vinawatosheleza
kuku wote. Vyombo hivi ni vizuri vifanyiwe usafi wa mara kwa mara, ili kuwaepusha
kuku na magonjwa. Maji machafu huwa ni chanzo kikuu cha magonjwa hasa ya kuhara.
Hakikisha kuku wako wanabadilishiwa maji angalau mara mbili kwa siku.
Mpya zaidi Nzee zaidi