Maelfu ya wafanyakazi Marekani waandamana kupinga ukosefu wa usawa


Maelfu ya wafanyakazi wa Marekani wamegoma kazi na kufanya maandamano wakipinga dhulma na ukosefu wa usawa.
Waandamanaji katika maandamano hayo yaliyopewa jina la "Mgomo kwa Ajili ya Maisha ya Watu Weusi", wametaka kuboreshwa hali ya ajira na mazingira ya kazi ya Wamarekani weusi. 
Maandamano hayo yaliyofanyika jana katika zaidi ya miji 24 ya Marekani yametayarishwa na jumuiya za wafanyakazi na taasisi za kutetea haki na uadilifu wa mbari zote. 
Watayarishaji wa maandamano hayo wametangaza kuwa, wapinzani wa dhulma na ukosefu wa usawa ambao hawakuweza kushiriki kwenye maandamano walinyamaza kimya kwa dakika kadhaa kuwaenzi na kuwakumbuka Wamarekani weusi waliouawa kikatili na polisi ya Marekani.

Mjini New York, maelfu ya waandamanaji hao walikusanyika mbele ya "Hoteli ya Kimataifa ya Trump" na kutangaza upinzani wao dhidi ya ubaguzi wa rangi unaofanyika kwa mpangilio maalumu na ukosefu wa usawa wa kiuchumi nchini Marekani.
Wamarekani wamekuwa wakifanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakipinga ukatili wa polisi na ubaguzi wa rangi. Maandamano hayo yalianza baada ya polisi mzungu kumuua Mmarekani mweusi, George Floyd hapo tarehe 25 Mei katika mji wa Muneapolis.
Mpya zaidi Nzee zaidi