Schauble ataka Umoja wa Ulaya kuwa na umoja wa kiuchumi


Spika wa Bunge la Ujerumani, Wolfgang Schauble amezitaka nchi wanachama za Umoja wa Ulaya kuwa na ujasiri wa kuanzisha muungano wa kifedha wenye nguvu na kutanua kundi la nchi zinazotumia sarafu ya euro kuwa umoja wa kiuchumi.

 Hayo ameyaandika katika gazeti la Ujerumani la Frankfurter Allgemeine Zeitung, kama mchangiaji mwalikwa. Schauble amesema hawapaswi kuikosa tena fursa hiyo na kwamba Ulaya ingekuwa mbali zaidi kama wazo la kuanzisha shirika la fedha la Ulaya lingefanikiwa mwaka 2010 wakati wa mzozo wa kifedha wa Ugiriki. 

Amesema Ulaya inahitaji ujasiri ambao haukuwa nao mwaka 2010 na kwamba janga la virusi vya corona ni sababu tosha kwa nchi za Umoja wa Ulaya kuungana pamoja. Schauble amesema Umoja wa Ulaya unatakiwa kulitumia janga la COVID-19 kujiuliza kile wanachoweza kukifanya kuwa bora zaidi kwa ajili ya mustakabali wa Ulaya.