WHO yasema Covid 19 ndilo janga baya zaidi kuwahi kulikumba shirika hilo la afya

Shirika la Afya Duniani WHO limesema janga la virusi vya corona linaloutikisa ulimwengu ambapo watu milioni 16 wameathirika kwa sasa ndilo janga baya zaidi shirika hilo kukabiliana nalo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia mkutano na waandishi wa habari uliofanywa kwa njia ya video huko Geneva, Uswisi, amesema kufuata masharti yaliyowekwa kudhibiti janga hilo ndio njia ya pekee inayoweza kuliangamiza.

Mkuu wa dharura katika shirika hilo la afya Michael Ryan kwa upande wake amezisifu Canada, China, Ujerumani na Korea Kusini kwa kulidhibiti janga hilo.

"Nchi ambazo zimetekeleza hatua za udhibiti zimepunguza kiwango cha kusambaa kwa virusi. Hatua hizo zinapoondolewa, virusi hivyo vinarudi. Kilicho wazi hapa ni kwamba shinikizo kwa virusi hivyo vinapelekea idadi kushuka na unapoondoa shinikizo basi idadi inaweza kupanda tena."

Kurudi tena kwa virusi hivyo katika nchi tofauti zikiwemo hata zile zilizofikiria kwamba zimeangamiza virusi hivyo ni mambo yanayoishangaza dunia huku idadi ya vifo ikikaribia kufika 650,000.

Mpya zaidi Nzee zaidi