Na Hamisi Nasri, MASASI
MGOMBEA ubunge jimbo la Masasi mjini kwa chama cha ACT-Wazalendo,Musa Mwadewa amewaomba viongozi wa vyama vya siasa wilayani Masasi mkoani Mtwara kufanya siasa safi na zenye kujali maslahi ya taifa na kuepuka kuendesha siasa za matusi kwenye majukwaa ambazo zinalenga kuchochea vurugu zisizo na tija.
Aliyasema hayo jana wilayani Masasi mkoani hapa mara baada ya kukabidhiwa fomu za kugombea ubunge jimbo la Masasi mjini katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo,ambaye pia ni mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Masasi,Gimbana Ntavyo
Alisema lengo la kufanya siasa ni kulijenga taifa kuwa kitukimoja na sio kuendesha siasa ambazo zinaweza kuchochea kuwapo kwa vurugu ambazo hazina tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Mwadewa alisema kuwa hakuna anayehitaji kuwa na kiongozi ambaye atakuwa chanzo cha kuwapo kwa machafuko kwa sababu ya siasa bali kila mmoja anahitaji kuishi kwenye nchi ambayo ina amani,utulivu na upendo.
Alisema ACT-Wazalendo kitahakikisha kinafanya uchaguzi ambao ni safi na wenye busara katika kuzungumza na wananchi kwenye majukwaa ili waweze kukipa nafasi ya kuongoza jimbo hilo la Masasi.
“Hatuhitaji vurugu hatuhitaji kuona nchi hii ndio inakuwa ya kwanza katika kusababisha machafuko kwa ajili ya siasa hasa kipindi katika kuelekea kwenye uchaguzi oktoba 28 mwaka huu sisi ACT-Wazalendo tunahitaji kuona kila kiongozi anasimamia majukumu yake kwa usahihi,”alisema Mwadewa
Alisema kwa mtazamo wake ni kwamba uchaguzi huu unakwenda kuleta mabadiliko makubwa ya nchi kwa vile wananchi wengi wanatarajio makubwa ya kuona wanapata vingozi waliobora na sio bora viongozi.watakaowaletea maendeleo.
Mwadewa alisema chama cha ACT-Wazalendo kinahitaji ushirikiano wa karibu kutoka Tume ya taifa ya uchaguzi pamoja na viongozi wa siasa wa vyama vingine hasa kuhakikisha kuona uchaguzi huo unakwenda vizuri kwa amani na utulivu.
Alisema iwapo nchi ikipata viongozi waliobora watasaidia kuwasimamia wananchi vema katika kuletea maendeleo yao pamoja na kulinda maslahi ya taifa na kwamba yeye wakipewa ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Masasi ataweza kuwaletea maendeleo.
