MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa Mjini Unguja Talib Ali
Talib amewataka wanafunzi wa shule ya Msingi ya Jumuiya ya Wazazi ya
Amani mkoa huo kutojiingiza katika masuala ya siasa kwenye uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akikabidhiwa vifaa vya ujenzi kwa ajili
ya ukarabati wa shule hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja
wa Wazazi wa tawi la Shangani Kiran Mawji Nathoo mjini Unguja.
Mwenyekiti huyo aliwataka wanafunzi hao kuacha masuala ya kujiingiza
kwenye siasa na badala yake waendelee kusoma na mambo ya siasa
waachiwe watu wakubwa.
"Tuachieni sisi watu wakubwa tuwahakikishieni tunawawekea chama
bora katika serikali ili muweze kupata mafanikio makubwa kwenye mambo
ya elimu,"alisema
Alisema mnachotakiwa kutambua ni kuwa CCM ni chama ambacho kinatimiza
ndoto na kiu za watanzania kwa kuwaletea maendeleo huku akitolea mfano
jumuiya ya wazazi ambayo inatoa elimu kupitia shule zake kwa watu wote
bila ya kujali itikadi ya chama wala dini.
"Nampongeza sana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Tawi la Shangani
kuja kutoa msaada huu ni jambo la pekee kuona kiongozi wa ngazi hiyo
ya kutoa msaada huu katika shule ya wazazi kwa kuona jukumu lake akiwa
kama mwanachama wa jumuiya hii kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa
mazuri ya kusomea kwa wanafunzi hawa hili ni suala la kuiga mfano
sana,"alisema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa tawi la Jumuiya ya Umoja wa Wazazi wa
tawi la Shangani Kiran Mawji Nathoo mjini Unguja alisema akiwa kama
mwanachama wa jumuiya hiyo ataendelea kutoa msaada wa aina yeyote kwa
ajili ya kuboresha mazingira ya shule za jumuiya ya wazazi.
Alisema pia atahakikisha anatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya
kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira ya kurizisha ili
waweze kupata elimu bora.
"Mimi ninaunga mkono juhudi za viongozi wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa
Taifa Rais Dk.John Magufuli na Makamu Mwenyekiti wake Rais Dk.Ali
Mohamed Shein katika hatua hizi za kuhakikisha sera za serikali zote
mbili na chama kuhusu elimu zinatekelezeka ndio maana nimeamua
kujitolea msaada huu katika shule hii ya Jumuiya ya wazazi,"alisema
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi ya Jumuiya ya Wazazi ya Amani
Khamis Kheria Ame alisema anashukuru kwa msaada huo na kwamba
ataendelea kuhakikisha shule hiyo inakuwa bora zaidi visiwani
Zanzibar.
"Msaada huu utasaidia katika shule yetu kufanya maboresho zaidi
ili iwe na hadhi ya kuwa ni miongoni mwa mali ya tasisi ya jumuiya ya
Wazazi hivyo CCM ni chama kubwa lazima shule hii nayo iwe na muonekano
mzuri ambao unaoendana na hadhi ya chama,"alisema
