Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo ameitaka jamii kupatiwa elimu ya mazingira ili wawe na utaratibu wa kuweka usafi katika mazingira wanayoishi.
Wito huo ameutoa huko Mbweni wakati alipokuwa akizungumza na vikundi vya usafishaji vya WAJAMAMA ambayo ni kampuni inayoweka akinamama na watoto katika hali ya usafi na kuwa na afya bora wakishirikiana na Safisha Zanzibar kwa lengo la kuona mji unakuwa safi na unavutia .
Amesema jamii inaona labda usafi ni wa Serikali peke yake au manispaa dhana hiyo indoshwe kwani kila binaadamu au kiumbe chochote kinahitaji kuwa na mazingira ya usafi sehemu anayoishi hivyo jitihada za kutoa elimu zinahitajika zaidi.
Hata hivyo amesema iwapo usafi utakuwemo nchini maradhi ya mripuko hayataweza kutokea Bajeti ya dawa itapungua uchumi utaongezeka kwa sababu wananchi watakuwa na afya nzuri na hilo ndio lengo la Serikali.
"Iwapo usafi utadumishwa jamii itaishi kwa kuwa na afya njema itaepukana na maradhi ya mripuko na ndio azma ya Serikali yetu", alisema Waziri huyo.
Aidha amesema mji unapokuwa safi mazingira yanapendeza hata watalii wataongezeka vijana watapata ajira na pato la Serikali litaongezeka.