Kenya yafungua anga lake kwa Tanzania

 

Serikali ya Kenya kwa mara ya kwanza tangu kuanza janga la Covid-19 imewajumuisha raia wa Tanzania katika orodha ya nchi ambazo wasafiri wake hawatalazimika kukaa karantini watakapowasili nchini humo.

Hatua hii inatazamwa kama hatua tata wakati Tanzania ikiwa bado haijatoa taarifa yoyote kuhusu maambukizi ya virusi vya corona kwa miezi kadhaa na Rais wake, John Magufuli, alitangaza kuwa ugonjwa huo umekwisha Tanzania.

Baada ya miezi kadhaa ya mvutano kuhusu namna ambavyo nchi hizo mbili zinavyoshughulikia janga la corona, sasa mambo yanaonekana kupoa.

Katika orodha mpya ya nchi ambazo Kenya imeruhusu raia wake kuingia bila kukaa karantini, Tanzania pia imeorodheshwa.

Nchi nyingine ni Afrika Kusini, Marekani, India, Mexico na Uhispania, ambazo ni miongoni mwa nchi zilizo na idadi kubwa ya maambukizi duniani kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani, WHO

Kwa muda sasa serikali ya Kenya ilihofia kuwa Tanzania haiko wazi kuhusu namna inavyoshughulika kupambana na janga la corona.

Rais wa Tanzania John Magufuli alitangaza kuwa ugonjwa huo umekwisha na hivi sasa kuvaa barakoa na kutochangamana ni suala nadra nchini humo.

Hatahivyo, mamlaka za Kenya zinataka wageni wote watakaoingia kuwa na nyaraka maalum zinazoelezea kama wana maambukizi au la

Kenya imethibitishwa kuwa na maambukizi ya watu zaidi ya 36,000 na vifo vya zaidi ya watu 600.

Post a Comment

0 Comments