Na Omary Mngindo, Kilangalanga.
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Michael Mwakamo, ameelezea kusikitishwa kwake kutokana na vitendo vya kurudishwa nyumbani wanafunzi wanaodaiwa hela ya chakula.
Aidha amewataka wazazi na walezi kutokukubaliana kwa baadhi ya mambo ambayo baadae yanakwenda kuwagharimu wenyewe, kwani makubaliano hayo mwisho wa siku yanakuwa sheria, hivyo kuwageukia kisha wanabaki kulalamika,
Mwakamo ameyasema hayo katika Vitongoji vya Kilangalanga, Janga na Mtongani akizungumza na wakazi kwenye mkutano wa Kampeni, ambapo alisema kuwa kurudishwa kwa wanafunzi kisa hela ya chakula binafsi kinamkera.
"Nitakapochaguliwa nafasi hii niliyoiomba kuna mengi ya kuyafanyiakazi, lakini na hili la wanafunzi kurudishwa nyumbani kwa kukosa hela ya chakula nitapambana nalo, kama ni kosa lipo kwa mzazi, sasa unapokwenda kumwadhibu mwanafunzi uoni kama unamuonea?, alisema Mwakamo.
Akizungumzia mikakati ya kupamabana na kadhia hiyo, Mwakamo alisema dawa yake kujengwa sekondari maeneo ya karibu, hali itayowapatia fursa wanafunzi kuweza kukimbia nyumbani kula kisha kutejea shule, jambo ambalo Ilani ya 2020/2025 imeliona hilo na kwenda kulifanyiakazi.
"Ilani yetu iliyopitishwa na viongozi wetu ngazi za juu chini ya Jemedali wetu John Magufuli imesheheni mambo mbalimbali yanayokwenda kutekelezwa, serikali inayoongozwa na chama chetu kwa kipindi cha miaka mitano sote mashahidi kazi kubwa zimefanyika na zinaendelea," alisema Mwakamo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilayani hapa Ludovic Remy aliwataka wana-Kibaha Vijijini kutorubunika kwa wagombea wanaotokea vyama vingine kwani ilani ya chama chao zinatekelezeka.
"Tunawaona wanasiasa wenzetu wanakuja kunadi sera zao, tuwasikilize lakini mwisho wa siku tuwachague wanaotokea chama chetu ambacho kina sera inayotekelezeka ukilinganisha na vyama vya wenzetu," alisema Ludovick.
