Ubelgiji imeunda serikali mpya hii leo, miezi 16 tangu uchaguzi ambao haukutoa mshindi wa wazi, ambapo waziri wa muda wa fedha Alexander De Croo ameteuliwa kuwa waziri mkuu mpya.
Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo, vyama saba kutoka maeneo yanayozungumza Kifaransa na Kidachi vilikubaliana kuunda muungano kuchukua nafasi ya serikali ya muda iliyokuwa inaongozwa na Sophie Wilmes, iliyoteuliwa mwezi Machi, mwanzoni mwa mlipuko wa janga la virusi vya corona.
Ubelgiji haijawa na serikali kamili tangu Desemba 2018, wakati muungano tawala wa vyama vinne uliposambaratika.
Vyama viwili vikubwa zaidi, chama Kisoshalisti cha wanaozungumza Kifaransa, na kile cha Wanaozungumza Kiflemi cha N-VA, wamepambana kuondoa tofauti zao, na kuuacha muungano wa vyama saba unaojulikana kama Vivaldi, kuwa chaguo pekee.
Serikali ya De Croo itaanza kazi rasmi kesho Alhamisi, wakati yeye na mawaziri wenzake watakapoapishwa na mfalme Philippe.
