Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ameahidi kuisaidia Iraq katika mapambano ya kulisambaratisha kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Merkel ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara ya waziri mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi mjini Berlin.
"Tunajua pia kwamba kundi linalojiita Dola la Kiislamu au Daesh bado halijaisha. IS inaendelea kuwa kitisho kwa kanda, na mbali ya kanda hiyo.
Ujerumani itaendelea kuisaidia Iraq katika mapambano dhidi ya IS na katika kuituliza nchi hiyo kupitia mfumo wa muungano wa kimataifa dhidi ya IS na pia ujumbe wa NATO nchini Iraq, alisema Merkel.
Jeshi la Ujerumani Bundeswehr, lina wanajeshi karibu 270 nchini Iraq, waliopelekwa kupambana dhidi ya Dola la Kiislamu nchini humo na katika nchi jirani ya Syria.
Katika wiki ijyo, wabunge wa Ujerumani wanatarajiwa kuidhinisha urefushaji wa mamlaka hii kwa miezi mingine 15, kwa ajili ya wanajeshi 500.
Kundi la Dola la Kiislamu lilidhibiti maeneo makubwa ya kaskazini mwa Iraq kati ya 2014 na 2017, lakini lilifurushwa kwa msaada wa muungano wa kijeshi ulioongozwa na Marekani, ambao uliihusisha pia Ujerumani.
