Kamishna wa masuala ya fedha wa Umoja wa Ulaya Mairead McGuiness, amesema umoja huo unaendeleza dhamira yake ya kufikia makubaliano ya kibishara na Uingereza baada ya Brexit, na kiongozi wa majadiliano Michel Barnier yuko tayari kwenda London kuongeza nguvu mazungumzo.
Uingereza imesimama kidete kwa kulikataa pendekezo la Umoja wa Ulaya la kujadili rasimu ya maandishi ya kisheria ya makubaliano ya biashara, hadi pale kutakapokuwa na mabadiliko makubwa.
Hali hii imeibua wasiwasi wa mchakato mzima kuishia kwa vurugu, kwa Uingereza kuondoka bila makubaliano.
McGuiness amesema mlango wa Umoja wa Ulaya unasalia wazi hadi dakika za mwisho, lakini akaongeza kuwa muda umekuwa mfupi sana.
Umoja wa Ulaya na Uingereza kila mmoja anamlaumu mwingine kwa kukwamisha majadiliano, na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alifahamisha wiki iliyopita kuwa nchi hiyo iko tayari kuondoka bila makubaliano.
