Wanajeshi wa Tigray wafyatua makombora katika jimbo jirani la Amhara

 


Wanajeshi wa jimbo la Ethiopia la Tigray wamefyatua makombora leo kuelekea mji wa Bahir Dar katika jimbo jirani la Amhara lakini hayajasababisha majeruhi wala uharibifu. 

Hayo ni kwa mujibu wa serikali ya Amhara, wakati vikosi vya serikali ya Addis Ababa vikielekea mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle. 

Ofisi ya mawasiliano ya serikali ya Amhara imesema kundi la Ukombozi wa Watu wa Tigray - TPLF lilifyatua makombora hayo usiku wa manane kuamkia leo. 

Amhara ambayo ina mzozo wa muda mrefu wa mpaka na Tigray, imewatuma wanajeshi wake kuviunga mkono vikosi vya serikali ya shirikisho. 

Wakati huo huo, Mkuu wa shirika la Afya duniani WHO Tedros Ghebreyesus amekanusha madai yaliyotolewa na mkuu wa jeshi la Ethiopia, kuwa anaongoza juhudi za kuwapatia silaha na msaada mwingine viongozi wa mkoa wa Tigray unaokabiliwa na operesheni ya kijeshi inayoendeshwa na serikali kuu. 

Ghebreyesus ambaye ni raia wa Ethiopia amesema madai hayo hayana ukweli na kwamba yeye binafsi anaunga mkono upatikanaji wa amani na kutoa wito kwa kila upande kupunguza mvutano kwenye mzozo unaendelea.


Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items